Mwakinyo atamba kumchapa Gonzalez

23Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwakinyo atamba kumchapa Gonzalez

BONDIA nyota wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo, anatarajia kupanda ulingoni kuzichapa na Sergio 'El Tigre' Gonzalez wa Argentina katika pambano la kimataifa litakalofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa mikataifa wa Kenyatta jijini hapo.

Mwakinyo ambaye anadhaminiwa na Kampuni ya Michezo wa Kubahatisha ya SportPesa Tanzania, jana alishiriki katika zoezi la kupima uzito lililosimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa ya Kenya (KPBC).

Akizungumza na gazeti hili jana baada ya kumaliza kupima uzito, Mwakinyo alitamba kushinda pambano hilo kutokana na maandalizi aliyofanya chini ya kocha wake, Tony Bellew na kudhaminiwa na SportPesa Tanzania.

Mwakinyo alisema kuwa hawezi kuwaangusha Watanzania na wakazi wa Afrika Mashariki na kuahidi kumchapa mpinzani wake kwa staili ya ‘knockout’ (KO).

“Sina sababu ya kutoa visingizio kuwa sijajiandaa vizuri. Wadhamini wangu, Kampuni ya SportPesa wameniandaa vizuri sana, kuwa chini ya kocha mzuri na kambi ya kisasa, ili niweze kufanya mambo makubwa zaidi, lazima nishinde pambano hili,” alisema Mwakinyo.

Mtanzania mwingine, Fatuma Zarika ‘iron’ atapanda ulingoni kutetea taji lake la ubingwa wa Baraza la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBC) wa uzito wa Super Bantam kwa kupambana na Catherine Phiri kutoka Zambia.

Habari Kubwa