Mwakinyo kuwania mikanda ya dunia

16Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwakinyo kuwania mikanda ya dunia

BONDIA bingwa wa mabara wa uzito wa Super welter, Hassan Mwakinyo anatarajia kupanda ulingoni kutetea mkanda wake wa Chama cha WBF katika pambano litakalofanyika Novemba 13, mwaka huu dhidi ya Jose Carlos Paz kutoka Argentina.

Na Adam Nyangasa, TUDARCo

Mbali ya kutetea mkanda huo, Mwakinyo pia atawania ubingwa wa mabara wa uzito huo huo wa Chama cha IBA. Pambano hilo limepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Next Door Arena.

Mapambano hayo yamepewa jina la Dar Fight Night na yameandaliwa na Kampuni ya Jackson Group Sports.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Kelvin Twissa, alisema siku hiyo mabondia kutoka nchi tano watapanda ulingoni katika mapambano ya utangulizi akiwamo aliyekuwa bingwa wa dunia wa WBC, Fatuma Zarika kutoka Kenya ambaye atavaana na Patience Mastara wa Zimbabwe.

Twisa alisema bondia mwingine Mtanzania na mtoto wa kiungo wa zamani wa Simba, Zulfa Yusuph Macho atapigana na Alice Mbewe wa Zimbabwe wakati Abdallah Pazi maarufu Dullah Mbabe atacheza dhidi ya Alex Kabangu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Alisema wameamua kuingia kwenye mchezo wa ngumi kutokana na kutambua vipaji vya mabondia mbalimbali hasa Mwakinyo ambaye anafanya vizuri katika mapambano yake.

"Tulifanya kazi na Mwakinyo kwa miaka mitatu na kuona ufanisi wake, tumeamua kuendelea naye na mabondia wengine wa Tanzania, tutaubadili mchezo wa ngumi nchini," Twissa alisema.

Naye Mwakinyo alisema ni fursa kwake na amejipanga kufanya vyema katika pambano hilo.

"Namshukuru Twissa na Kampuni ya Jackson Group Sports ambao wameonyesha nia ya kuubadili mchezo wa ngumi za kulipwa, sitawaangusha Watanzania," alisema Mwakinyo.

Mwakilishi wa WBF Tanzania, Chatta Michael alisema kuwa rais wa shirikisho hilo, Goldberg Howard ndiye atasimamia mapambano hayo.

Habari Kubwa