Mwakyembe, Kiwale kupanga mikakati

08Nov 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Mwakyembe, Kiwale kupanga mikakati

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Sunday Kiwale, anatarajia kukutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa malengo la kujadili maandalizi ya safari yake ya kuelekea nchini Uingereza, imefahamika.

Kiwale anatarajia kuondoka nchini ifikapo Novemba 24, mwaka huu kwa ajili ya kwenda kupigana na Tommy Frank, katika pambano la kuwania ubingwa wa IBO, raundi 12, ambalo litakalofanyika Novemba 29, mwaka huu, nchini humo.

Akizungumza na gazeti hili jana, baada ya kumaliza mazoezi yake ya asubuhi kwenye viwanja vya Shule ya Uhuru, Kiwale alisema kuwa anaamini kikao chake na Mwakyembe kitamsaidia kumjenga zaidi.

“Mwakyembe aliniambia anataka kukutana na kuzungumza na mimi kabla ya kusafiri kwenda Uingereza kwa ajili ya pambano langu, naamini nikikutana naye atanipa mbinu nyingi ambazo zitanisaidia katika pambano hilo," alisema Kiwale.

Bondia huyo aliongeza kuwa anaendelea vema na programu za maandalizi kwa ajili ya pambano hilo na anajiamini atakwenda kufanya vizuri, lakini akihitaji Watanzania wazidi kumwombea dua ili aweze kuipeperusha vema bendera ya taifa.

“Naomba Watanzania wenzangu wazidi kuniombea na kunisapoti ili niweze kuiwakilisha vema bendera ya Tanzania, nimejipanga vizuri, sina hofu na mpinzani wangu, japo kuwa ninakwenda kupigana kwao,” alisema Kiwale.

Bondia huyo ananolewa na kocha, Rajabu Mhamila maarufu Super D, ambaye aliliambia gazeti hili kuwa Kiwale atarejea nyumbani na mkanda wa pambano hilo.

Habari Kubwa