Mwakyembe mgeni onyesho la vitenge

17Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Mwakyembe mgeni onyesho la vitenge

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe anatarajia kushiriki katika onyesho maalumu la mavazi ya vitenge litakalofanyika Jumamosi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Onyesho hilo litakaloshirikisha wanamitindo zaidi ya 40, limeandaliwa na Mbunifu wa mavazi  hapa nchini,  Ally Rehmtullah kwa kushirikiana na Kampuni ya Hightech Wear na Flygle ya China.

Akizungumza jana jijini, Rehmtullah, alisema lengo la onyesho hilo ni kuitangaza nchi kwenye vazi la kitenge na pia kudumisha ushirikiano baina ya Tanzania na China pamoja na kutangaza biashara ya mavazi.

“Hili ni onyesho litakalo wajumuisha wanamitindo takribani 40 watakaonyesha mavazi mbalimbali ya vitenge, tumeamua kushirikiana na kampuni ya “JININGA” katika kuandaa onyesho hili la vazi la kitenge kutokana na kampuni hii kuwa msambazaji mkuu wa aina hiyo ya nguo haoa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla,”  alisema Rehmtullah.

Alisema ili kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa ndani na nje na nchi katika masuala ya ubunifu wa mavazi, mitindo na ushonaji, kampuni yake itashirikiana na kampuni hiyo kutengeneza nguo kutoka China.

“Kampuni yetu inaamini kuwa kupitia onyesho hili, hamasa itaongezeka kwa kuwa kila washiriki kuanzia washonaji, wanamitindo, watengenezaji wa vitenge kutoka China, na hadhira ya kariba mbalimbali, wataongea na vyombo vya habari kuhusu vivutio tulivyonavyo na umahiri wa Watanzania kuhusu ubunifu wa mavazi wa kutumia vitenge,” aliongeza Rehmtullah.

Naye Msemaji wa Hightech Wear na Flygle Tanzania, Aoron Tian Zhonghua, alisema wamekuja nchini kuwekeza kama walivyofanya katika nchi nyingine barani Afrika na pia waliamua kushirikiana na Rehmtullah ili kuongeza soko la biashara kupitia vazi la kitenge.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Vivian Shalua, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo, alisema lengo kuu la onyesho hilo ni kuwaweka karibu wabunifu wa mavazi na wanamitindo na watengenezaji wa vitenge kutoka China na kutoa nafasi wawekezaji hao kujifunza mambo mema yaliyoko nchini Tanzania.

“Lengo kubwa la onyesho hili ni kufungua viwanda ili tualike wawekezaji waweze kufungua viwanda ndani ya Tanzania na pia kutambulisha zaidi vazi la vitenge nchini na kuthamini vazi la vitenge ambalo litakuwa la nguo za aina mbalimbali,” alisema Shalua.

Habari Kubwa