Mwambusi: mabeki wetu walitubeba

12Nov 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Mwambusi: mabeki wetu walitubeba

YANGA juzi walifanikiwa kupunguza pengo la pointi baina yao na Simba baada ya kuifunga Ruvu Shooting kwa magoli 2-1, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi ameimwagisa sifa safu ya ulinzi ya timu hiyo kwa kufanikisha ushindi huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwambusi, alisema kuwa uimara wa safu yao ya ulinzi chini ya mabeki Kelvin Yondani na Andrew Vincent 'Dante' umeiepusha timu yao kupoteza pointi mbele ya Ruvu Shooting waliocheza vizuri kwenye mchezo huo.

"Tunashukuru kwa pointi hizi tatu ambazo zinatufanya tuendelee kusogea kileleni, wapinzani wetu walicheza vizuri sana na kama sio uimara wa mabeki wetu basi mambo yangekuwa tofauti," alisema Mwambusi.

Mwambusi alisema kwenye mchezo huo wachezaji wake walianza kwa kusuasua na kutanguliwa kufungwa lakini walifuata maelekezo yao makocha na kubadilika kipindi cha pili.

"Lakini pia niseme wenzetu Ruvu Shooting walijitahidi kutubana na kutupa presha kwenye mchezo wetu ila ilikuwa lazima tupate pointi tatu na tumefanikiwa," alisema Mwambusi.

Katika hatua nyingine, Mwambusi alimlalamikia mwamuzi wa mchezo huo, Mathew Akrama kwa kutochezesha kwa haki mchezo huo.
"Mliokuwapo uwanjani mmeona, maamuzi yake yalikuwa ya kutatanisha, wachezji wakigusana anatoa faulo..., waamuzi wetu lazima wabadilike kwa kweli," alisema Mwambusi.

Alisema wanatarajia kupumzika kwa muda mfupi kabla ya kuingia tena kambini kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi hiyo utakaonza mwezi ujao baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

Habari Kubwa