Mwanamama 'kuzihukumu' Yanga, Simba Jumamosi

17Feb 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwanamama 'kuzihukumu' Yanga, Simba Jumamosi

KWA mara ya pili refa wa kimataifa mwanamke anayetambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Jonesia Rukyaa anatarajiwa kusimama katikati kuchezesha mechi ya mzunguko wa pili ya watani wa jadi Yanga na Simba itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mwamuzi Jonesia Rukyaa (kulia) akimuonyesha kadi ya njano mchezaji

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine alisema Rukyaa atasaidiwa na Josephat Bulali kutoka Tanga na Samuel Mpenzu wa Arusha.

Mwesigwa alimtaja mwamuzi wa akiba katika mchezo huo, ambao Yanga watakuwa wenyeji kuwa ni Elii Sasii wa Dar es Salaam huku Kamisaa ni Khalid Bitebo 'Zemberwa' kutoka jijini Mwanza.

Hata hivyo, tofauti na ilivyo kawaida, jina la refa huyo na wasaidizi wake halikuwekwa hadharani kama ilivyo taratibu za kuwaweka kwenye orodha majina ya waamuzi na mechi watakazochezesha.

"Miaka yote waamuzi wa Simba na Yanga hupangwa mapema katika ratiba lakini safari hii kamati ilishindwa kuafikiana juu ya nani achezeshe hiyo mechi, lakini kesho (leo) Kamati itakaa tena kupanga," kilisema chanzo chetu.

Taarifa za ndani kutoka TFF zinaeleza kuwa Rukyaa alikuwa amepangiwa mechi nyingine ya ligi hiyo kati ya Stand United dhidi ya JKT Ruvu ya mkoani Shinyanga ambayo sasa atapangiwa refa mwingine.

Mechi ya kwanza ya Rukyaa kuchezesha watani hao wa jadi ilikuwa ni Nani Mtani Jembe iliyofanyika mwaka juzi na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Wakati huohuo, Shirikisho la Soka Tanania (TFF) limetangaza viingilio vya mechio ya watani wa jadi, ambao Sh.7000 ndiyo kiingilio cha chini.

Kiingilio cha juu cha mchezo huo kitakua Sh. 30,000 kwa VIP A, Sh. 20,000 VIP B na C, Sh. 10,000 (Chungwa) na Sh. 7,000 (Bluuna kijani)