Mwanariadha anayelilia kambi Olimpiki

08Feb 2016
Nipashe
Mwanariadha anayelilia kambi Olimpiki

"TUSIPOANZA kambi ya maandalizi ya michuano ya michezo ya Olimpiki mapema mwezi huu, itakuwa vigumu kurejea na medali katika mashindano hayo, kutokana na kwamba tunakutana na wanariadha waliofanya maandalizi, muda mrefu".

mwanariadha Alphonce Felix

Hayo ni maneno ya mwanariadha Alphonce Felix aliyefuzu kushiriki michezo hiyo iliopangwa kufanyika Agosti mwaka huu jijini Rio de Janairo nchini Brazil.

Felix anasema Tanzania imekuwa na hulka ya kufanya maandalizi ya zimamoto, jambo ambalo linawatesa wanariadha wa timu ya taifa wanapokutana na wale waliokaa kambini muda mrefu kufanya maandalizi ya mashindano hayo.

Anasema imekuwa vigumu kutekeleza suala la kambi jambo linalopelekea kuwakatisha tamaa wanariadha kujitokeza kutokana na kuihofia hali ya kutelekezwa hadi dakika za majeruhi ndipo kambi inaanza.

Mwanariadha huyo anasema kambi ya miezi miwili bado haitoshi, angalau inatakiwa mwanariadha akae miezi sita au nane, hapo unaweza kufanya jambo la maana katika mashindano.

"Serikali inapaswa ijiulize kwanini kila mashindano Tanzania haifanyi vizuri?
Hii ni kutokana na maandalizi duni tunayofanya," akafafanua.

Akitolea mfano wanariadha wanariadha wanariadha wa zamani waliofanikiwa kuliletea sifa taifa, Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na wengine, amesema Serikali inapaswa kurudi nyuma kujua walifanya nini mpaka wakafikia hivyo.

Anasema awali timu ya riadha na michezo mingine, ilikuwa ikijaliwa sana ikiwemo kuanza kambi mapema, na vipaji kuanza toka wakiwa mashuleni jambo ambalo lilileta tija, tofauti na ilivyo sasa, kambi zimekuwa za zimamoto, kitendo ambacho kinakatisha tamaa wanariadha wanaoenda kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo.

"Ifike wakati Tanzania ing'are katika michezo ya kimataifa, na si kusindikiza kila siku na kuonekana kichwa cha mwendawazimu, wakati uwezo wa kulitatua suala hilo upo," anasema kwa masikitikoo.

Ukiacha hilo, Felix amesema serikali inapaswa kujiuliza kwanini wanariadha wakishiriki mashindano ya kujitegemea wanafanya vizuri, na hii ni kutokana na maslahi wanayopata, tofauti wakiwa kwenye timu ya taifa.

"Unapewa dola 100, ambazo hazitoshi kuzigawanya kwenye familia, zingine zibaki kwa ajili ya matumizi pale unapokuwa nje katika mashindano ya kimataifa, unawezaje kushinda?" Akahoji.

Anasema kwenye kikosi cha timu ya taifa wengi hawafanyi vizuri, ni kutokana na kukata tamaa, kwa sababu haiwajali.

Hata hivyo, pamoja na hayo yote, amesema bado serikali haijachelewa kwa mwaka huu, lakini isifanye mzaha kwa wanamichezo waliofuzu, iwaweke kambini mapema ili iwe rahisi kwenda kufanya vizuri katika michezo hiyo.

Bila ya kufanya hivyo, anasema wanariadha wengi watakuwa wakishindwa kumaliza mbio zao kwa wakati kutokana na kuchoka mapema, kwa kukimbizwa na wale ambao wana mazoezi ya muda mrefu.

Kutokana na hilo, ameliomba Shirikisho la mchezo huo nchini (RT), kujiwekea mikakati mapema, ya kuhakikisha kambi ya timu ya taifa ya riadha inaanza mapema, kama wanahitaji kurudisha mchezo huo katika hadhi yake.
"Riadha sio lelemama, inatakiwa maandalizi makubwa ili wanariadha waweze kufanya vizuri katika mashindano hayo," anasisitiza mwanariadha huyo.

Moja ya changamoto kubwa zinazowakabili ni pamoja ukosefu wa posho wakati wakiwa kambini, kutokana na kwamba familia zinakuwa zinasumbua kudai pesa za matumizi ili hali wao hawajalipwa.

Felix ambaye amefuzu mara kadhaa katika mashindano ya kimataifa, msimu huu amepania kufanya vizuri, ili aweze kurejea na medali katika mashindano ya michezo hiyo, hivyo amewataka wahusika nao kutekeleza majukumu yao.

Habari Kubwa