Mwisho wa Morrison Simba?

14May 2022
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwisho wa Morrison Simba?
  • …Klabu yatangaza kumpumzisha, mwenyewe ajibu asema kwa moyo mzito anatangaza kuwa nje kwa mechi zote zilizobaki …

KLABU ya Simba imempa mapumziko hadi mwisho wa msimu huu mchezaji wake Bernard Morrison.

Bernard Morrison.

Taarifa iliyotolewa jana na klabu hiyo kwenye mtandao wake rasmi wa Instagram imesema kuwa klabu imefikia maamuzi hayo baada ya pande zote mbili kukubaliana kwa lengo la kumpa nafasi kupumzika na kushughulikia mambo yake binafsi.

Aidha, klabu hiyo imemshukuru kwa mchango mkubwa kwa kipindi chote alichohudumu ndani ya timu hiyo.

"Tunatambua na kuthamini mchango wa Morrison katika miaka miwili aliyotumikia klabu yetu na kuisaidia kupata mafanikio kadhaa, ikiwemo kucheza robo fainali ya michuano ya Afrika mara mbili, kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ubingwa wa Kombe la FA, na Mapinduzi.

“Kwa mchango na mafanikio hayo, klabu inamshukuru mchezaji huyo kipenzi cha Wanasimba kwa kujitoa kwake kuipigania klabu yake," iliandika taarifa hiyo ambayo ilionyesha imetolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo ambaye ni Barbara Gonzalez.

Simba imemtakia kila la kheri winga huyo katika mapumziko yake na safari yake ya soka hapo baadaye.

Dakika chache baada ya taarifa hiyo, Morrison mwenyewe kupitia ukurasa wake wa facebook alisema: “Kwa Moyo mzito natangaza kwamba, nitakuwa nje ya uwanja kwa msimu uliobaki kutokana na matatizo ya kifamilia ambayo yako nje ya uwezo wangu na yanaweza kuathiri kiwango changu kwa timu kama nitaiwakilisha klabu. Mengi yanahitajika kusemwa kuhusu hilo, lakini naweza tu kuitakia kila la heri klabu katika mechi zetu zilizobaki. Nina matumaini na kusali ili mambo yangu yaishe haraka inavyowezekana ili ili niweze kujiunga tena na timu.”

Morrison, mmoja kati ya wachezaji watukutu nchini ndani na nje ya uwanja, alisajiliwa na klabu hiyo msimu miwili iliyopita akitokea Yanga.

Hata hivyo usajili wake ulisababisha mvutano mkubwa kiasi cha Yanga kuamua kumpeleka kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, akidaiwa kuwa alikuwa na mkataba wa klabu hiyo, huku mwenyewe akidai hakuwa nao, hivyo kusaini mkataba wa Simba.

Alishinda kesi hiyo mwaka 2020, lakini klabu ya Yanga haikukubali, ikaamua kulipeleka kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Kesi za Michezo Duniani (CAS), ambako kesi iliunguruma, huku akiwa anaitumikia klabu yake mpya, na akaibwaga tena.

Februari mwaka huu, alisimamishwa kwa utovu wa nidhamu kwa kile kilichodaiwa kutoroka kambini.

Pamoja na kuitumikia na kuipa mafanikio Simba na vituko vya hapa na pale, Morrison alishindwa kuitumikia timu hiyo mara mbili pale ilipotakiwa kwenda kucheza nchini Afrika Kusini na timu za Kaizer Chiefs na Orlando Pitates kwa nyakati tofauti kutokana na kuwa na matatizo na Idara ya Uhamiaji nchini humo.

Habari Kubwa