MZFA: Alliance FC, Mbao mjitathmini

25Mar 2020
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
MZFA: Alliance FC, Mbao mjitathmini

CHAMA cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), kimezitaka timu zote za mpira wa miguu zinazoshiriki ligi mbalimbali mkoani humo kuhakikisha zinafanya tathmini katika ushiriki wao wa ligi ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara jambo ambalo linaweza kuzinusuru na janga la kushuka daraja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Katibu Mkuu wa MZFA, Leonard Malongo, alisema baadhi ya klabu hapa nchini hazipo katika nafasi katika ushiriki wao wa ligi, hivyo ni muhimu kufanya tathmini kwa muda huu wakati ligi zikiwa zimesimama kutokana na hofu ya kuenea kwa virusi vya corona.

Alisema timu za mkoani hapa ambazo zinashiriki Ligi Kuu, Alliance FC na Mbao FC, zipo katika hali mbaya kutokana na kutokuwa katika nafasi nzuri, hivyo bila jitihada za kufanya tathmini ya kina na kurekebisha kasoro zilizojitokeza hali itaweza kuwa mbaya zaidi.

Pia Malongo aliwataka wadau wa soka mkoani hapa kuhakikisha wanazisaidia kwa hali na mali timu zote ili ziweze kushiriki ligi zao kwa kuzichangia fedha zitakazozisaidia kukidhi mahitaji yao hususan safari kutoka kituo kimoja hadi kingine, lakini kuwawezesha viongozi kutoa posho kwa wachezaji ili kuongeza morali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Alliance FC, Yusuph Budodi, alisema kwa sasa wana vikao vya ndani na nje kwa ajili ya mipango mikakati ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwa mechi zilizobaki, hivyo aliwatoa hofu wadau wa soka na kuahidi michezo iliobaki kufanya vizuri.

“Tuna mechi sita za nyumbani na tatu za nje, tutahakikisha kila mechi kwetu ni fainali, hivyo tumejipanga na tutaendelea kujipanga, lakini tunahitaji kupangwa na kupanguliwa kwa mawazo ya watu ambao wapo nje ya klabu na waliopo ndani tunahitaji mawazo sana hasa kipindi hiki kigumu,” alisema Budodi.

Katika msimamo wa Ligi Kuu timu hizo za Mwanza zipo katika mstari wa kushuka daraja kufuatia Alliance kushika nafasi ya 18 ikiwa na pointi 29 zilizotokana na mechi 29, wakati Mbao FC iliyoshuka dimbani mara 28 hadi sasa ikiwa nafasi ya 19 na pointi 22.

Habari Kubwa