Mzizima, Arusha, Iringa zachuana

06Jul 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Mzizima, Arusha, Iringa zachuana

CHAMA cha Mbio za Magari Tanzania (AAT), kimesema kimepokea maombi kutoka katika klabu tatu nchini zinazohitaji kuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka huu, imeelezwa.

Ofisa Uhusiano wa AAT, Athumani Hamisi, ameliambia gazeti hili klabu zilizoomba kuandaa michuano hiyo zinatoka katika mikoa ya Arusha, Iringa na Mzizima ya jijini, Dar es Salaam.

Hamisi alisema katika maombi yao, klabu hizo zimethibitisha zinauwezo wa kusimamia michuano hiyo kikamilifu.

Alisema waliamua kuanza maandalizi ya michuano hiyo baada ya kupata ruhusa ya kuendelea na mashindano kutoka katika Baraza la Michezo Tanzania (BMT).

"Morogoro wametujulisha hawawezi kuandaa mashindano ya mwaka huu kwa sababu wamekwama katika masuala la kifedha, tumewaelewa na tutashirikiana nao wakati mwingine wakiwa tayari," alisema Hamisi.

Aliongeza klabu ya Mount Usambara na Dar es Salaam hazijarudisha majibu kwa chama hicho juu ya kueleza na nafasi yao.

Alieleza ratiba ya mashindano hayo itatangazwa hivi karibuni baada ya kukamilika kwa sehemu ya mchakato wa maandalizi.

Habari Kubwa