Nabi atwaa tuzo, Mugalu mchezaji bora

28Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Nabi atwaa tuzo, Mugalu mchezaji bora

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ametwaa tuzo ya kocha bora wa Julai, huku mshambuliaji wa Simba, Chris Mugalu akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ilimalizika Julai 18.

Taarifa iliyotolewa jana na Bodi ya Ligi, Nabi na Mugalu ndio waliong’ara kwa mwezi huo.

Nabi, aliisaidia Yanga kushinda mechi mbili za Julai, ikiwafunga Ihefu FC na Simba, huku ikitoka suluhu na Dodoma Jiji.

Kocha huyo alijiunga na Yanga Aprili baada ya klabu hiyo kumtimua Cedric Kaze na tangu atue amekuwa msaada mkubwa wa kikosi hicho hadi kumaliza ikiwa kwenye nafasi ya pili.

Mugalu amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi huo baada ya kuwashinda Charles Ilamfya wa KMC na Juma Luzio wa Mbeya City.

Mchezaji huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), aliyesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Power Dyamos ya Zambia, alifunga mabao matano mwezi huo akiisaidia Simba kushinda mechi tatu na ikapoteza moja.

Wachezaji ambao wamechukua tuzo kwa msimu huu ni Prince Dube wa Azam, Septemba, Mukoko Tonombe wa Yanga, Oktoba, John Bocco wa Simba, Novemba, Saido Ntibazonkiza wa Yanga, Desemba, na Deogratius Mafie wa Biashara United, Januari.

Wengine ni Anuary Jabir wa Dodoma Jiji, Februari, Luis Miquissone wa Simba, Machi, Claotus Chama pia wa Simba, Aprili.
Dude alirudia tena Mei, huku Bocco akiibeba pia Juni.