Nabi awapa Makambo, Mukoko kazi maalum J'2

10Sep 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Nabi awapa Makambo, Mukoko kazi maalum J'2
  • ***Ni katika kuhakikisha Rivers United haichomoki kwa Mkapa, huku Kibwana naye akitawa...

BAADA ya taarifa mbaya ya kuwakosa nyota wake watatu katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria Jumapili wiki hii, haraka Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amepata suluhisho na kutoa majukumu maalum ili kuhakikisha wanapata ushindi mnono katika ....

mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Juzi Yanga iliweka wazi kuwa wamepokea taarifa kutoka Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), kuwa hawataruhusiwa kuwatumia wachezaji wao wa tatu, kiungo Mganda Khalid Aucho, beki wa kulia, Mkongomani Shabani Djuma na straika Fiston Mayele ambaye ni raia wa DR Congo, sababu ikiwa ni wote kuchelewa kupata Hati za Uhamisho wa Kimataifa, ITC.

Hata hivyo, haraka Nabi amepata suluhisho la wachezaji hao baada ya kutumia muda wake mazoezini kwa kuwaandaa na kuwapa majukumu maalum, Heritier Makambo katika nafasi ya ushambuliaji na Mukoko Tonombe kwenye kiungo mkabaji.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo, Nabi amewapa majukumu baadhi ya wachezaji huku Mukoko akipewa majukumu mazito ambayo alikuwa akitarajiwa kupewa Aucho.

Mtoa habari wetu alisema kwenye safu ya ushambuliaji ambayo awali alipewa Mayele ambaye katika michezo miwili mfululizo ya kirafiki, ameonyesha uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu, kazi hiyo sasa imeelekezwa kwa Makambo huku pia Yacouba Songne na Yusuf Athuman nao wakiwekwa sawa kwa kuongezewa makali.

"Djuma, Aucho na Mayele walikuwa kwenye mipango ya Kocha Nabi, lakini baada ya sakata la kutopata ITC ya nyota hao, mwalimu ameamua kuwapa majukumu wachezaji wengine.

"Kazi kubwa aliyotakiwa kufanya Aucho kwa namna inavyoonekana mazoezini ni wazi ataendelea nayo Mukoko ambaye yuko fiti, huku eneo la Djuma likibaki kwa Kibwana Shomari baada ya kufanya vizuri kwa msimu uliopita," alisema.

Kwa upande wa Msemaji wa Yanga, Haji Manara, alisema kuhusu kambi ya timu hiyo inaendelea vizuri, kuelekea mchezo huo na kwamba hawana presha kwa kukosekana kwa wachezaji hao kwa kuwa tayari Nabi amepata mbadala wa nyota hao watakaoikosa mechi hiyo.

"Kila kitu kinaenda vizuri na tayari kocha Nabi, anaendelea kufanya kazi yake, tunatarajia kupata matokeo mazuri na kusonga mbele kwenye michuano hiyo," alisema Manara.

Yanga itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Rivers United, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili kabla ya timu hizo kurudiana nchini Nigeria Septemba 18, mwaka huu.

Timu itakayopata matokeo ya jumla kwenye mechi hizo mbili, itakutana na mshindi wa jumla kati ya Al-Hilal ya Sudan na Fasil Ketema ya Ethiopia, ambazo nazo zitashuka dimbani Jumapili.