Nabi awapa walinzi majukumu Yanga SC

10Dec 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Nabi awapa walinzi majukumu Yanga SC
  • … Ni katika kuhakikisha wanapata ushindi mzuri dhidi ya Simba na…

KUELEKEA mechi ya watani zao Simba itakayochezwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Kocha Mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi amewapa majukumu mabeki wake na kuwataka kuwa makini ili kuweza kuzuia safu ya ushambuliaji ya wapinzani wao.

Safu ya ulinzi ya Yanga inaongozwa na mabeki wa kati, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Djuma Shaban (kushoto), David Bryson (kulia) na Shomari Kibwana ambaye ni kiraka mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbili kwa ufasaha wa hali ya juu.

Kocha Nabi amesema kulingana na ugumu wa mechi hiyo ana imani itakuwa ya ushindani na safu ya ushambuliaji ya wapinzani wao itaingia kivingine kwa kuhakikisha wanatafuta ushindi dakika za mwazoni.

Alisema wakati kila mchezaji akipewa majukumu yake kuelekea mchezo huo pia amewasisitizia mabeki wake kuwa makini kwa kuwadhibiti washambuliaji wa Simba.

“Safu ya ulinzi tayari inajua majukumu yake, washambuliaji nao wanaelewa nini wanatakiwa kufanya katika mchezo huu, ambao utakuwa wa kiufundi na kimbinu zaidi kwa kila upande,” alisema Nabi.

“Tunawaheshimu sana Simba, tunajua ubora na madhaifu yao, tunajiandaa kwa ajili ya kwenda kutafuta pointi muhimu katika mchezo huo,” aliongeza.

Alisema kuhusu kikosi chake hasa kwenye safu ya ulinzi ana imani kila mmoja ana uwezo mkubwa na kufanya vizuri katika mchezo huo kulingana na maandalizi ambayo wanayafanya.

Habari Kubwa