Namungo FC yazibeba timu Ruangwa kupitia SportPesa

25Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Namungo FC yazibeba timu Ruangwa kupitia SportPesa

KAMPUNI ya michezo ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa Tanzania, imesema kufanya vizuri kwa Namungo FC kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara ndiko kumewavutia wao kumwaga vifaa vya michezo Ruangwa mkoani Lindi.

SportPesa wiki iliyopita ilikuwapo mkoani humo kwa ziara fupi ya ugawaji vifaa vya michezo kutoka klabu za Uingereza ambazo kampuni hizo zinazidhamini kupitia Kampeni yake ya Kits for Afrika.

Katika ziara yao hiyo, SportPesa iliwagawia vifaa hivyo timu nane za Ruangwa ikiwamo mipira ya kisasa na yenye ubora inayotumiwa na klabu hizo kubwa baadhi zikiwa ni Hull City na Everton.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Uwekezaji na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, alisema hawajutii udhamini walioutoa kwa Namungo ambayo kwa sasa ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Tarimba alisema Namungo inastaili pongezi nyingi kutokana na kupanda kucheza Ligi Kuu msimu huu na kufanya vizuri na hiyo ni kutokana na ubora wa timu hiyo.

“Ninaitabiria Namungo kufanya vizuri zaidi katika misimu mingine ijayo, kama imeweza kuwa katika nafasi nne za juu ikiwa ni msimu wa kwanza tangu ilipopanda.

“Hivyo hatujutii udhamini huu tulioutoa kwa Namungo kutokana na kutuwakilisha vema kwenye ligi kwa nafasi waliyopo kwenye msimamo.

“Namungo imetushawishi kuja kutoa msaada wa vifaa vya michezo kwa timu nyingine zinazoshiriki ligi mbalimbali, lengo likiwa ni kuona zinapatikana timu nyingine kama ilivyokuwa Namungo hapa Ruangwa,” alisema Tarimba.

Habari Kubwa