Namungo, Ihefu zatishana Bara

08Apr 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Namungo, Ihefu zatishana Bara

NYASI za viwanja viwili zinatarajia kuwaka 'moto' katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo Namungo FC itawakaribisha Ihefu FC kwenye Uwanja wa Kassim Majaliwa wakati Mbeya City itawavaa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili, Kocha Mkuu wa Namungo FC, Hemed Morocco alisema wamefanya maandalizi mazuri kuelekea mchezo huo na kikosi kipo tayari kukabiliana na wapinzani wao kutoka jijini Mbeya.

Morocco alisema mechi hiyo itakuwa ya ushindani kwa sababu timu zote zinahitaji kupata matokeo chanya ili kujiweka katika nafasi nzuri ya uhakika wa kubakia kwenye ligi hiyo.

"Hautakuwa mchezo rahisi, kwa sababu kila mmoja wetu anatafuta matokeo mazuri, tutaingia uwanjani kwa kuwaheshimu wapinzani wetu, tuko nyumbani tunahitaji kutumia vizuri uwanja wa nyumbani, pia wenzetu wanatafuta matokeo mazuri," alisema Morocco.

Naye Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Zuberi Katwila alisema wanahitaji pointi tatu muhimu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuendelea kubaki katika ligi hiyo.

Katwila alisema timu yake iko katika nafasi mbaya kwa sasa wanahitaji kupambana zaidi ili kuondoka na pointi tatu na hatimaye kujinasua kwenye nafasi waliyopo kwenye msimamo wa ligi hiyo.

"Nimewaambia wachezaji wanapaswa wajiamini na tupambane kuhakikisha tunapata pointi tatu kwenye mechi zetu zilizobakia ikiwamo dhidi ya Namungo FC, haitakuwa rahisi ukizingatia kila timu kwa sasa inahitaji pointi," alisema Katwila.

Habari Kubwa