Namungo yaapa kurudi nafasi ya tatu

13May 2022
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Namungo yaapa kurudi nafasi ya tatu

KIKOSI cha Namungo leo kinashuka kwenye uwanja wa nyumbani, Ilulu mjini Lindi kucheza dhidi ya Mbeya Kwanza, huku ikiapa kutaka kurejea kwenye nafasi ya tatu ambayo itaifanya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo Jamhuri Kihwelo 'Julio' amesema tayari ameshaliandaa jeshi lake kwa ajili ya kusaka pointi tatu, ili kurejea tena kwenye nafasi hiyo ambayo wanaitaka kwa udi na uvumba.

"Haitokuwa mechi rahisi, wao wanataka ushindi ili wasishuke daraja na sisi tunataka nafasi hiyo ili kukaiwakilishe nchi kwenye michuano ya kimataifa, itakuwa mechi ngumu sana, lakini tumejiandaa kwa hilo," alisema Julio.

Naye straika wa timu hiyo Jacob Massawe amesema wachezaji wote wa Namungo wamepata mshtuko, kwani baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba walikuwa kwenye nafasi ya tatu, lakini kwa sasa wameshuka hadi nafasi ya sita kutokana na timu zingine kushinda, hivyo mshtuko huo umewapa morali a kupambana ili kushinda mechi ya leo na kurejea kwenye nafasi yao ya awali.

Iwapo itashinda leo, Namungo yenye pointi 30, itaiengua Azam yenye pointi 32 na kukaa juu yake, lakini nafasi ya tatu wiki hii itategemea na matokeo kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Geita Gold, mechi iliyochezwa jana.

Kama Geita Gold yenye pointi 31 ikishinda, itakwea kwenye nafasi ya tatu kwa pointi 34, hivyo hata Namungo ikishinda itakaa kwenye nafasi ya nne.

Mbeya Kwanza ndiyo timu inayoshika mkia kwa sasa ikiwa na pointi 21 kwa michezo 22 ambayo imeshacheza.

Ni ushindi tu ndiyo utawaweka kwenye matumaini ya kuweza kuepuka janga hilo.

Habari Kubwa