Namungo yaitangazia vita Sahare FA

04Jul 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Namungo yaitangazia vita Sahare FA

NAMUNGO FC imesema inaionea huruma Sahare All Stars kwa 'kupotea njia' kutokana na kichapo watakapokutana katika mechi ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA itakayofanyika Julai 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, Tanga.

Sahare All Stars :PICHA NA MTANDAO

Ofisa Habari wa Namungo FC, Kindamba Namlia, aliliambia gazeti hili kwa sasa hawafikirii kabisa mechi hiyo na mashabiki wao wanauwaza mchezo wa fainali utakaochezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

"Ni kweli mashabiki wetu watakwenda mjini Tanga kutupa hamasa, lakini wengi zaidi wamesema wao wamejiandaa zaidi kwenda Sumbawanga kwa sababu wanajua kikosi chetu hakiwezi kusumbuliwa na wenyeji wetu," alisema Namlia.

Kiongozi huyo alisema lengo la Namungo msimu huu ni kuona timu hiyo inakata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa na si vinginevyo.

"Tumejipanga kisawasawa, ni kama mtu aliyeamua kufanya kazi ya kuchinja, ina maana akiwa machinjioni kitu kitakacholetewa na mteja basi tunachinja tu, hatuangalii rangi wala saizi, Sahare wamekuja, ni bahati mbaya sana kwao. Tunachofanya kwa sasa ni kuwakatia pasipoti wachezaji wetu ambao hawana kwa ajili ya kusafiri kuelekea mechi za kimataifa," alisema ofisa huyo.

Safari ya Namungo kwenye michuano hiyo inayotoa mwakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), ilianza kwa kuichapa Might Elephants bao 1-0, halafu wakawafunga Green Warrios goli 1-0 baadaye wakaiadhibu Biashara United mabao 2-0 na kuifunga Mbeya City mabao 2-1  na kuwachapa Alliance goli 1-0.

Timu hiyo pia imekuwa ikifanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kucheza mechi 16 sasa bila kupoteza, ikishika nafasai ya nne katika msimamo ikiwa na pointi 56.

Habari Kubwa