Namungo yaleta mapinduzi Bara

09Jul 2020
Somoe Ng'itu
Lindi
Nipashe
Namungo yaleta mapinduzi Bara

IKISHIRIKI Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Kocha Mkuu wa Namungo FC, Thierry Hitimana, amesema timu yake imefanikiwa kuleta mapinduzi kwenye ligi hiyo ambayo hutoa mwakilishi wa nchi katika mashindano ya kimataifa.

Watoto wanaookota mpira wakinawa kabla ya kuanza kwa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa mkoani Lindi.

Akizungumza na Nipashe mjini hapa, Hitimana alisema kikosi chake kimeleta mabadiliko na kuongeza ushindani katika Ligi Kuu Tanzania Bara katika msimu wake wa kwanza.

Hitimana alisema anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana katika kila mechi waliyocheza na kufanikiwa kutimiza malengo yao wa asilimia zaidi ya 80.

Kocha huyo alisema haukuwa msimu rahisi, lakini juhudi za pamoja za viongozi, wachezaji na wadau wa timu hiyo zimesaidia kufanya vema na ikiwa ni moja ya timu zinazoogopewa.

"Tumefanikiwa kufanya vizuri na kuamsha wengine, tumeleta mapinduzi katika Ligi Kuu, naamini tumekosa ubingwa, lakini tuna nafasi ya kupata tiketi ya kwenda kushiriki mashindano ya kimataifa ya CAF (Shirikisho la Soka Afrika)," Hitimana alisema.

Kutokana na kuipa mafanikio Namungo FC, kocha huyo anatajwa kuwindwa na Yanga, ili kuungana na Mbelgiji Luc Eymael kwa mara nyingine.

Namungo iko katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA, itavaana na Sahare All Stars Jumapili mchana wakati jioni Simba itapambana na Yanga. 

Habari Kubwa