Namungo yatajwa kuivuruga Yanga

08Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Namungo yatajwa kuivuruga Yanga

ILI kukabiliana na ushindani katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa 2019/20, uongozi wa Namungo FC ya Lindi, unatajwa kuwa kwenye mazungumzo ya kumsajili kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili, imeelezwa.

Namungo FC

Tayari Namungo FC imefanikiwa kumsajili mshambuliaji wa Alliance FC, Bigirimana Blaise kwa kumpa mkataba wa mwaka mmoja.

Taarifa kutoka jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa tayari Namungo na Kabwili wameanza mazungumzo na endapo golikipa huyo wa zamani wa Serengeti Boys yatakamilika, atasaini mkataba na timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu ili aongeze nguvu katika kikosi chao.

Habari kutoka Yanga zinasema kuwa kwa sasa Kabwili ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake wa awali wa miaka miwili na timu hiyo iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera.

"Sisi tunajipanga kujiimarisha, na taarifa rasmi tulizonazo ni kuwa Kabwili ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika, huku hakuna kiongozi aliyemwita kukaa mezani kuzungumzia usajili wake," alisema kiongozi mmoja wa Namungo.

Ofisa Habari wa Namungo, Kidamba Namlia, alisema kuwa klabu yao imejipanga kusajili wachezaji wenye uwezo na uzoefu ambao utawasaidia kufanya vema katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

"Ligi Kuu inaushindani sana, ili tuweze kuimudu ni lazima tusajili wachezaji wenye nguvu na watakaotupa matokeo mazuri, hatutaki kuona tunasindikiza wengine, tumejiandaa kuja kushindana," Namlia alisema.

Klabu hiyp pia imewaongezea mkataba wachezaji wake wengine watatu ambao ni pamoja na Jukumu Kibanda, Lusajo Reliants na Daniel Joram.

Habari Kubwa