Nape akemea vyama vya michezo vinavyokwepa kufanya uchaguzi

05Apr 2016
Gurian Adolf
Sumbawanga
Nipashe
Nape akemea vyama vya michezo vinavyokwepa kufanya uchaguzi

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ameziagiza ofisi za makatibu tawala wa mikoa nchini, kuhakikisha wana visimamia vyama vya michezo vya mikoa ili kuondoa urasimu wa kiuongozi unaosababisha vyama hivyo kushindwa kusimamia michezo kwa manufaa ya umma.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Alisema hayo jana wakati akizungumza na wadau wa Sekta ya Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa mkoa huo (RDC) uliopo mjini hapa.

Alisema baadhi ya vyama vya michezo vya mikoa hususani soka, vimekuwa na urasimu kiasi cha kutengeneza mazingira ya kutofanya chaguzi za viongozi na kuitisha mikutano mikuu ya wananchama kwa mujibu wa katiba zao.

"Nasikia hapa Rukwa, watu hawataki kuitisha mikutano ya kikatiba kwa zaidi ya miaka miwili wala kujaza nafasi za uongozi zilizo wazi kwa madai kuna waraka kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao ni siri sasa waraka gani unakuwa siri," alihoji Nnauye.

Kauli ya waziri huyo ilikuja baada ya mdau, Lusungu Kihahi kuhoji uhalali wa baadhi ya viongozi wa Rurefa kutofanya mikutano mikuu ya kikatiba kwa zaidi ya miaka miwili, pia TFF kutoa waraka ambao wajumbe wa mkutano mkuu walielezwa ni wa siri ukitaka nafasi za zilizo wazi za uongozi zisijazwe hadi mwaka 2017 uchaguzi wa viongozi utakapofanyika tena.

Habari Kubwa