Nape asisitiza programu za vijana

27Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Nape asisitiza programu za vijana

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye amesema kuendeleza programu za michezo kwa vijana ndiyo njia pekee ya kusaka maendeleo.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye

Nape alisema hayo jana katika uzinduzi wa msimu wa sita wa mashindano ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars.

Waziri huyo pia aliwapongeza Airtel Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na Shirikisho la Soka nchini (TFF) za kukuza mchezo huo wenye mashabiki wengi duniani.

“Programu za soka za vijana ndiyo muhimili wa maendeleo ya soka popote pale duniani. Ndiyo maana nasisitiza umuhimu wa mashindano ya Airtel Rising Stars ambayo matunda yake yameonekana dhahiri katika kipindi cha miaka mitano iliyopita”, alisema Nape.

Alisema mashindano hayo yanayoshirikisha wachezaji chipukizi pia wamesaidia katika kuinua soka la wanawake, baadhi ya wachezaji walioibuliwa na michuano hiyo waliitwa kujiunga na timu ya Taifa (Twiga Stars).

Aliongeza kuwa kupitia michuano hiyo, baadhi ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza zimenufaika na mashindano hayo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano alimhakikishia waziri huyo kuwa kampuni hiyo ina nia thabiti ya kuendelea kudhamini michuano hiyo ambayo imesaidia kuzalisha wachezaji chipukizi hapa nchini.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa