Nape kuongoza Tulia Marathon leo

11Mar 2017
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Nape kuongoza Tulia Marathon leo

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za 'Tulia Marathon' ambazo zinafanyika leo kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa imeelezwa.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa mbio hizo ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Akson alisema kuwa mbio hizo zitahusisha wanariadha maarufu, viongozi wa kitaifa, wananchi wa kawaida pamoja na wabunge kutoka majimbo mbalimbali ya hapa nchini.

"Kuna baadhi ya wabunge watashiriki mbio hizi kwa kutoa fedha lakini kutakuwa na wabunge kama watano hivi ambao mtawaona wakikimbia kesho (leo) pale Sokoine na wao watakimbia kilomita tano, Waziri wetu mwenye dhamana ya michezo, Nape ndiye atakuwa mgeni wetu rasmi,” alisema mratibu huyo.

Alisema licha ya washiriki wa michuano hiyo kuimarisha afya lakini lengo kubwa ni kupata kiasi cha Sh. milioni 121 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya afya kwa kuanzia kwenye Kituo cha Afya cha Ruanda kilichoko Mbeya Mjini, Hospitali ya Wilaya ya Rungwe na ukarabati wa baadhi ya majengo ya shule za sekondari ikiwamo Loleza.

“Tunawakaribisha wafanyabiashara, wanafunzi, vijana ,walemavu pamoja na watoto kuja kuonyesha vipaji vyao na pia michuano hii itawajengea afya,” aliongeza.

Aliongeza kuwa washiriki wengine kwenye mashindano hayo katika makundi maalum wakiwamo wazee, watoto na watu wenye ulemavu watachuana katika mbio za kilomita mbili.

Habari Kubwa