Ndanda, Lipuli  zavamia Simba

07Dec 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Ndanda, Lipuli  zavamia Simba

KLABU ya Ndanda FC ya Mtwara, imesema ina mpango wa kusajili wachezaji wawili kwa mkopo kutoka kikosi cha Simba katika dirisha hili dogo la usajili.

Mchezaji wa timu ya Simba, Juma Luzio anayewaniwa na timu ya Ndanda

Ndanda inaungana na Lipuli ambayo kupitia kocha wake, Seleman Matola, imekiri kutuma maombi ya kutaka kusajili wachezaji wawili kwa mkopo katika dirisha hili dogo.

Habari kutoka ndani ya uongozi wa Ndanda, zinasema tayari imetuma barua kwa uongozi wa Simba kuomba kumsajili kwa mkopo mshambuliaji Juma Luizio, ambaye ameshindwa kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kocha Joseph Omog.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Zesco ya Zambia, pia anawindwa na Lipuli inayonolewa na Matola.Alipoulizwa msemaji wa Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, Haji Manara, kama klabu hiyo imepokea barua ya Ndanda FC, alisema hana taarifa hizo.

Manara alisema kama kutakuwa na kitu chochote uongozi wa timu hiyo utatolea taarifa."Sifahamu kuhusu hilo, kama kuna jambo lolote ninakawaida ya kuzungumza na wanahabari... nitawaambia, lakini kuhusu hilo mimi sifahamu," alisema Manara.

Dirisha dogo la usajili ambalo lilifunguliwa Novemba 15 linatarajiwa kufungwa Desemba 15, mwaka huu.

 

Habari Kubwa