Ndayiragije bado asubiri mkataba

23Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ndayiragije bado asubiri mkataba

WAKATI Azam FC imetangaza kuachana na Etienne Ndayiragije, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa bado halijakamilisha mchakato wa kupata Kocha Mkuu mpya atakayekinoa kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Rais wa TFF, Wallace Karia picha mtandao

Rais wa TFF, Wallace Karia, alimesema hayo juzi na kuongeza kwamba bado wanasubiri ripoti ya Taifa Stars kutoka kwa Ndayiragije, ambaye amefanikiwa kuipeleka kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Karia alisema kuwa Watanzania hawapaswi kuwa na haraka juu ya uamuzi wa kocha mpya kwa sababu jambo hilo hutekelezwa kwa umakini.

Kiongozi huyo amekanusha uwepo wa taarifa kuwa TFF inatarajia kumpa mkataba rasmi kocha huyo, baada ya kuachana na klabu ya Azam FC.

"Nawaomba Watanzania wawe na subira, sisi bado hatujamtangaza kocha mpya wa Stars, Watanzania wanapaswa kuwa na subira, kama Azam walisema ni wao na si sisi, subirini," alisema Karia.

Aliongeza kuwa bado wanaendelea kupokea maombi kutoka kwa makocha mbalimbali, na mara baada ya mchakato huo kukamilika, wataweka wazi mrithi wa Mnigeria Emmanuel Amunike.

Habari Kubwa