Ndayiragije hesabu kali akiwavaa TP Mazembe

15Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Ndayiragije hesabu kali akiwavaa TP Mazembe

MABINGWA watetezi wa mashindano ya Kombe la Kagame, Azam FC wameahidi kufanya vema katika mchezo wao wa robo fainali dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) utakaochezwa kesho jijini Kigali, Rwanda.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Etienne Ndayiragije.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Azam FC, Etienne Ndayiragije, alisema kikosi chake kiko tayari kuwakabili mabingwa hao wa zamani wa Afrika na wamejipanga kwa kuongeza umakini katika mchezo huo.

Ndayiragije alisema kuwa ili waweze kusonga mbele katika mashindano hayo, watatakiwa kucheza kwa nguvu kwa sababu wanakutana na wachezaji wenye uzoefu wa mechi za mtoano.

"Tunashukuru tunaendelea vizuri na mazoezi, tunajua TP Mazembe ni wazoefu, tutajiandaa kuivaa Mazembe kutokana na timu hiyo ilivyo, kwanza tulikuwa na mpango wa kucheza na Rayon, lakini sasa tutajipanga kucheza na Mazembe, hii ni mechi ya dakika 90, ni mtoano, tunahitaji kujiandaa kufanye nini na kwa wakati gani, tuko tayari," alisema Ndayiragije.

Alisema kuwa kikosi chake kinaundwa na wachezaji mchanganyiko, hivyo anaamini watajituma kuhakikisha wanafanya vema hasa wakijua wao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo.

"Tunaomba mashabiki wetu pamoja na Watanzania wazidi kutusapoti na kutuombea ili tuweze kurudi nyumbani na kombe letu, tumeziangalia timu zote zinazoshiriki mashindano haya kuanzia hatua ya kwanza, tutajipanga kuhakikisha tunaendelea kufanya vema na kutetea ubingwa," Ndayiragije alisema.

Aliongeza kuwa mashindano ya msimu huu yana ushindani zaidi tofauti na misimu iliyopita kwa sababu timu zote zilijiandaa kuwania kombe hilo kuanzia hatua ya makundi.

Alieleza kuwa TP Mazembe ni moja kati ya timu bora barani Afrika, hivyo ni lazima unapokutana nayo, ucheze kwa heshima.

Habari Kubwa