Ndayiragije rasmi Stars? Aachia Azam

22Oct 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Ndayiragije rasmi Stars? Aachia Azam

UONGOZI wa Azam FC umemtangaza kocha wake wa zamani, Mromania Aristica Cioaba kuwa mrithi mpya wa Mrundi Etienne Ndayiragije, ambaye wameachana naye rasmi katika klabu hiyo.

Uamuzi wa Azam FC umefikia hatua hiyo baada ya kuona Ndayiragije anahitaji muda zaidi wa kukiandaa kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Satrs), ambayo amefanikiwa kuipeleka kwenye fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Cioaba aliwasili nchini juzi na jana alisaini mkataba mpya wa kuanza kuitumikia timu hiyo ambayo kesho inatarajia kukutana na mabingwa watetezi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin "Popat", alisema wanaamini uamuzi wao utakuwa na faida kwa nchi na wanamtakia Ndayiragije mafanikio zaidi akiwa na Taifa Stars.

Popat alisema Azam FC imempa mkataba wa mwaka mmoja Mromania huyo na endapo atafanya vizuri zaidi, wataendelea kuwa naye kwenye klabu hiyo.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa, tayari TFF ilishaanza kufanya mazungumzo na Ndayiragije, pamoja na Azam FC ambayo ndiyo ilikuwa na mkataba na kocha huyo.

Imeelezwa kuwa, tangu kutimuliwa kwa Mnigeria Emmanuel Amunike, TFF imeshapokea maombi zaidi ya 200 kutoka kwa makocha mbalimbali duniani ambao wameonyesha nia ya kuifundisha Taifa Stars.

Katika kikosi cha Taifa Stars, Ndayiragije anasaidiwa na Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda pamoja na Suleiman Matola kutoka Polisi Tanzania.

Baada ya kufuzu CHAN, kibarua kinachofuata cha Taifa Stars, ni kuikaribisha Equatorial Guinea, katika mchezo wa kwanza wa Kundi L wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuchezwa nchini Qatar mwaka 2022.

Habari Kubwa