Ndemla azitesa Simba, Yanga

24Mar 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Ndemla azitesa Simba, Yanga
  • ***Ni baada ya kiungo huyo kukataa kusaini mkataba mpya, safari yake ya kucheza soka Sweden sasa...

BAADA ya kukosa namba katika kikosi cha kwanza cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba, Said Ndemla amekataa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo na kuelekea Sweden kucheza soka la kulipwa, imefahamika.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinasema Ndemla ambaye mkataba wake na vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu, amewakatalia mabosi wake wa Simba kusaini mkataba ili kukamilisha mchakato wake wa kwenda kujiunga na klabu ya AFC Eskilstuna ya nchini humo.

Chanzo chetu kilisema kuwa Ndemla alifaulu katika majaribio lakini klabu hiyo ilikuwa tayari kumsajili akiwa ni mchezaji huru.

"Baada ya kuona nafasi ya kucheza ni ndogo na siku zinakwenda, Ndemla hakukubali kusaini, ameshawishiwa mara kadhaa kusaini, lakini amewakatalia viongozi, kubwa ni kutokana na kuwa na ahadi ya kusajiliwa Sweden, lakini kwa sharti la kuwa mchezaji huru," kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kiliongeza AFC Eskilstuma bado inamhitaji Ndemla baada ya miaka miwili iliyopita kushindwa kumsajili kutokana na dau la juu walilotakiwa kulipa ili kuvunja mkataba wake na Wekundu hao wa Msimbazi.

“Mkataba wa Ndemla upo ukingoni, hivyo hii ni nafasi ya kiungo huyo kwenda kucheza soka la kulipwa nchini humo kulingana na uongozi wa timu hiyo kumhitaji akiwa mchezaji huru,” alisema chanzo hicho.

Taarifa nyingine zinasema kuwa Yanga pia imetajwa kumwania kiungo huyo aliyepandishwa akitokea Simba B, lakini amekataa kutua Jangwani.

Kiongozi mmoja wa juu wa Yanga aliliambia gazeti hili kuwa wamefanya mawasiliano na kiungo huyo kwa nyakati tofauti, lakini aliendelea kushikilia msimamo wake wa kutosaini mkataba.

“Tuliona hii nafasi nzuri kwetu kumpata Ndemla kwani hapati nafasi katika kikosi cha kwanza, lakini tumeshindwa baada ya kutueleza kwamba mipango yake kwa sasa ni kucheza soka la kulipwa, hivyo huenda akaondoka baada ya msimu huu kumalizika, kwa sababu alifuzu majaribio,” alisema kiongozi huyo.

Klabu za Ligi Kuu nchini zimeonekana kutumia muda huu wa mapumziko kuanza mchakato wa usajili kwa lengo la kulinda nyota wake inaowahitaji.

Habari Kubwa