Ndugai kuongoza wabunge kuwashangilia Stars Afcon

15Jun 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Ndugai kuongoza wabunge kuwashangilia Stars Afcon

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, anatarajiwa kuongoza wabunge 83 kwenda kuishangilia Timu ya Taifa (Taifa Stars) katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu.

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai

Stars iko Kundi C na itaanza mechi yake ya kwanza Juni 23 mwaka huu dhidi ya Senegal wakati siku ya ufunguzi Misri itaikaribisha Zimbabwe.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Mwenyekiti wa Timu ya Bunge, William Ngeleja, alisema wabunge 83 wamejiorodhesha ili kushuhudia fainali hizo.

Ngeleja alifafanua kuwa kutokana na vikao vya Bunge kuendelea, wabunge hao wamegawanywa kwenye makundi mawili ambapo kundi la kwanza litaondoka Juni, 20 mwaka huu, kutokea jijini hapa kwenda kushiriki ufunguzi na mechi itakayochezwa Juni, 23 mwaka huu.

“Hili kundi litarejea Dodoma Juni 24, mwaka huu ili kuwahi zoezi la kuhitimisha mjadala wa bajeti Juni 25, mwaka huu na mara baada ya kumalizika, kundi la pili litaondoka Juni 26, mwaka huu na litarejea nchini Julai 2, mwaka huu na litaishia Dar es salaam kwa kuwa Bunge litakuwa limeahirishwa,” alisema.

Aidha, aliipongeza Taifa Stars katika mechi ya kirafiki iliyochezwa juzi dhidi ya Misri ambapo Misri (Mafarao) waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

“Tunaamini mechi hii imejenga msingi mzuri wa wao kushiriki fainali hizi,”alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Spika ambaye ni Mratibu wa safari hiyo, Saidi Yakubu, alisema Spika Ndugai ataongoza kundi la kwanza la wabunge litakaloshuhudia ufunguzi na mechi ya Taifa Stars dhidi ya Senegal.

Naye Kocha wa Timu ya Bunge, Venance Mwamoto, alisema wanaiombea timu hiyo ifanye vizuri lakini safari yao pia itatangaza vivutio vya utalii nchini na upatikanaji wa korosho.