Ngairo aipeleka Tembo Warriors Kombe la Dunia

02Dec 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Ngairo aipeleka Tembo Warriors Kombe la Dunia

MSHAMBULIAJI wa Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania kwa Watu wenye Ulemavu 'Tembo Warriors', Franck Ngairo, amekuwa mwiba mkali kwa timu pinzani wakati akitoa mchango mkubwa kwa kuiwezesha kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Uturuki.

Mshambuliaji hatari wa Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania kwa Watu wenye Ulemavu 'Tembo Warriors', Franck Ngairo, akimtoka beki wa Cameroon, wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 5-0 kwenye mechi hiyo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CANAF), iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jana. PICHA: JUMANNE JUMA

Ngairo ambaye juzi aliipeleka Tembo Warriors hatua ya robo fainali baada ya kuifungia bao pekee wakati ikishindi 1-0 dhidi ya Sierra Leone, jana aliendeleza moto wake wa kucheka na nyavu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Cameroon, hivyo kufuzu hatua ya nusu fainali, ambayo imewapa tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia mwakani.

Timu nne zilizofuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya Afrika kwa watu wenye ulemavu (CANAF), inayofanyika hapa nchini, zimefuzu moja kwa moja kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Uturuki na hadi gazeti hili linakwenda mitamboni zilizokuwa zimeshafuzu ni Tanzania na Ghana.

Mabao ya Tembo Warriors katika mchezo huo dhidi ya Cameroon, yalifungwa na Alfan Kiyanga dakika ya pili na 15, Ramadhan Chomelo dakika ya 18 kabla ya Ngairo kuhitimisha shughuli hiyo dakika ya 36 na 44.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana baada ya mchezo huo, Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa, alisema Tanzania ni mara yake ya kwanza kwenda kucheza Kombe la Dunia na timu ya Tembo Warriors ambao ni wenye ulemavu wa viungo, wameliheshimisha taifa katika anga za kimataifa, hivyo atatoa zawadi ya Sh. 200,000 kwa kila mchezaji kutoka mfukoni kwake kutokana na kutambua kazi kubwa waliyoifanya.

Alisema kitendo cha Tembo Warriors kuipeperusha vema bendera ya Tanzania ni somo na changamoto kwa timu zingine za Taifa kujitathmini na kutafakari wanapokosea kushindwa kufanya vizuri.

"Kwa mara ya kwanza Tanzania itacheza Kombe la Dunia, si haba kuingia huku kupitia soka la walemavu, Tembo Warriors wametupa soka na changamoto kwetu na timu zetu zingine za taifa, kwa wachezaji waliokamilika viungo kuelekea michuano ya kimataifa.

"Serikali itaendelea kusapoti na kujenga uwezo katika soka la watu wenye ulemavu, nina imani kuna mawakala hapa nchini kutoka mataifa mbalimbali wamekuja kuangalia wachezaji na tayari kuna taarifa kwamba baadhi ya wachezaji wetu wameangaliwa na kuweza kupata nafasi ya kwenda kucheza Misri, Uturuki hata Uganda," alisema Bashungwa.

Habari Kubwa