Ngasa awatuliza mashabiki Yanga

04Aug 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ngasa awatuliza mashabiki Yanga

WINGA wa Yanga, Mrisho Ngasa amewataka mashabiki wa timu hiyo wasiwe na hofu na kikosi chao kitakachoshiriki katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

WINGA wa Yanga, Mrisho Ngasa

Ngasa ambaye yupo na kikosi kilichoko kambini mkoani Morogoro, amesema kuwa pamoja na hali ngumu na changamoto mbalimbali wanazopitia katika klabu hiyo kwa sasa, kikosi chao kitakuwa imara na kitaonyesha ushindani kwenye ligi.

Winga huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Azam FC , Simba, Mbeya City na Ndanda za hapa nchini, alisema kocha wao ameweka programu nzuri za mazoezi na kila mchezaji anauchu wa kufanya vizuri.

"Mashabiki wasubiri kuona kazi uwanjani..., tunaendelea na mazoezi na kocha anafahamu mashabiki wanataka nini na mpaka kambi itakapomalizika tutakuwa vizuri," alisema Ngasa.

Nyota huyo aliyejiunga na Yanga akitokea Ndanda FC, anaamini kikosi chao kitarejea kwenye makali kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

" Haya ni mambo ya mpito..., Yanga tutarejea kwenye makali yetu yaliyozoeleka," alisema mchezaji huyo.

Yanga imeweka kambi Morogoro kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi USM Alger ya Algeria utakaofanyika Agosti 19 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa