Ngassa: Ligi ya Sauzi inatia uvivu, mapumziko marefu

31Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Ngassa: Ligi ya Sauzi inatia uvivu, mapumziko marefu

KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa ameanza kuichukia Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini kwa sababu ya mapumziko marefu.

Mrisho Khalfan Ngassa

Akizungumza na Lete Raha juzi kutoka Bethlehem, Ngassa alisema kwamba Ligi ya Afrika Kusini inamboa kwa sababu ya mapumziko marefu baada ya mchezo mmoja.

“Kwa mfano sasa hivi tulicheza mechi ya kwanza Agosti 23, lakini hatuchezi tena hadi Septemba 14, ni mapumziko marefu sana, yaani hadi mtu ile hamu inaisha. Ligi inapendeza ianchezwa mfululizo ndiyo tunaona hata Ligi za wenzetu Ulaya zipo hivyo,”alisema Ngassa.

Baada ya kufungwa 2-1 na Chippa United katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini, Free State Stars itashuka tena dimbani Septemba 14, kumenyana na Bloem Celtic Uwanja wa nyumbani, Goble Park.

Na haitachukua muda mredu kabla ya kurudi uwanjani kwa ajili ya mchezo wa tatu, kwani Septemba 21 watamenyana na Golden Arrows Uwanja wa James Motlatsi.

Katika mchezo wa kwanza, Ngassa alitokea benchi dakika ya 63 kwenda kuchukua nafasi ya Mbuyiselo Thethani wakati huo tayari FS imekwishpigwa 2-1, mabao ya wenyeji yakifungwa na Rhulani Manzini dakika ya tatu na 32, wakati la kwao lilifungwa na Charles Kampi dakika ya 13.

Ngassa yuko katika msimu wake wa pili Free State Stars tangu ajiunge na timu hiyo kama mchezaji huru kutoka Yanga SC ya Dar es Salaam.

Habari Kubwa