Ngoma atakiwa kufanyiwa upasuaji

16Mar 2016
Lasteck Alfred
Lete Raha
Ngoma atakiwa kufanyiwa upasuaji

STRAIKA wa Yanga, Donald Ngoma amedai kuwa kwasasa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa jicho lake la kushoto ambalo limekuwa likimsumbua huku likitiririsha machozi kila mara.

Straika huyo wa zamani wa Platinum FC ya Zimbabwe alisema, “ Ninaona vizuri, tena jicho linalotoa machozi linaona vizuri zaidi lakini siko tayari kufanyiwa upasuaji kwa sasa kwani ninahofia kuwa huenda ikanifanya nishindwe kucheza.

“Unajua nilipoenda majaribio nchini Sweden mwaka jana ndipo nilipoanza kupata tatizo hilo, niliporudi nyumbani daktari aliniambia kuwa moja ya chanzo kilikuwa ni baridi kali ya nchini Sweden na alinisihi kuwa nifanyiwe upasuaji ili hali ya kutiririsha machozi imalizike lakini siwezi.

“Nataka nicheze mpira kwani sijaona athari yoyote, pengine nitakapofanyiwa upasuaji nitaweza kushindwa ucheza vizuri kutokana na kutoona vizuri hivyo watu wasinifikirie kuwa huwa ninalia uwanjani.

“Mkiona ninatoa machozi si kwasababu ya furaha au machungu ni hali tu ya jicho langu kwasasa, ingawa ninatumia dawa na ninaamini linaweza kupona bila upasuaji,”alisema.

Ngoma amekuwa moja ya wachezaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha Yanga akiwa tayari amefunga mabao 13 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Habari Kubwa