Ngoma bado atakiwa Yugoslavia

24Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Ngoma bado atakiwa Yugoslavia

BAADA ya kucheza soka la kiwango cha juu na kufanikiwa kuifungia timu yake bao moja katika mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly straika wa kimataifa wa Yanga,

Donald Ngoma

Donald Ngoma bado anatakiwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Yugoslavia.

Taarifa ambazo Nipashe imezipata jana jijini Dar es Salaam zinaeleza kwamba bado klabu hiyo inamuhitaji Ngoma na inawataka mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kukubali kufanya nao mazungumzo.

Chanzo hicho kilisema kwamba katika barua yao ambayo wameituma tena kuwakumbusha Yanga juu ya kumuhitaji Ngoma, wamesema kwamba wako tayari kumnunua kwa dau la Dola za Marekani 350,000 (zaidi ya Sh. milioni 700 za Tanzania).

"Yule wakala bado anakumbusha barua yake kuhusiana na kumuhitaji Ngoma, lakini Yanga hawataki hata kukaa mezani kuzungumza, na wamesema wako tayari kuongeza dau endapo watatakiwa kufanya hivyo," kilisema chanzo chetu.

Kiliendelea kusema kwamba straika mwenyewe yuko tayari kwenda kujiunga na timu hiyo na anaitaka Yanga ikubali kufanya mazungumzo.

Endapo Ngoma atauzwa na kwenda kujiunga na klabu hiyo, atapata nafasi ya kucheza Ligi ya Europa msimu ujao. Mkataba wa Ngoma ambaye alitua Yanga akitokea FC Platinumz ya Zimbabwe unatarajiwa kumalizika mwakani.

Habari Kubwa