Ngoma, Niyonzima majanga Yanga

26Feb 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Ngoma, Niyonzima majanga Yanga
  • *** Nyota hao wataikosa mechi ya kesho ya Klabu Bingwa Afrika pamoja na kiungo Salum Tetela.

BALAA la majeruhi limeendelea kuiandama Yanga baada ya viungo, Haruna Niyonzima na Salum Telela kuumia na kuunga na straika wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma aliyefiwa kuikosa mechi ya kesho dhidi ya Cercle de Joachim.

Donald Ngoma akichanja mbunga.

Yanga, mabingwa mara 25 wa Tanzania Bara, kesho jioni watakuwa wenyeji wa timu hiyo ya Ligi Kuu ya Mauritius katika mechi ya marudiano ya raundi ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msemaji wa Yanga, Jerry Muro aliwaambia waandishi wa habari kuwa Niyonzima na Telela wataikosa mechi hiyo itakayosimamiwa na marefa kutoka Eritrea kutokana na majeraha waliyoyapata katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Simba na JKT Mlale.

Muro alisema Ngoma amefiwa na mdogo wake na aliondoka nchini jana na kurejea kwao Zimbabwe kuungana na familia yao katika mazishi.

"Timu inaendelea na mazoezi baada ya kumaliza mechi ya Kombe la Shirikisho, lakini tunasikitika katika mechi ya Jumamosi tutawakosa wachezaji wetu watatu; Ngoma aliyepata msiba, Niyonzima alipata majeraha katika mchezo wetu dhidi ya Simba. Salum Telela pia aliumia jana (juzi) wakati tunacheza na JKT Mlale (Kombe la FA)," alisema.

Msafara wa timu ya Cercle de Joachim ulitarajiwa kuwasili nchini jana jioni. Muro alisema kiingilio cha juu katika mechi hiyo kitakuwa ni Sh. 30,000 wakati cha chini kitakuwa Sh.5,000.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 13, Yanga walishinda 1-0, shukrani kwa bao pekee la Ngoma.

Habari Kubwa