Ninje aihofia Zanzibar Heroes

06Dec 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Ninje aihofia Zanzibar Heroes

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Ammy Ninje, amesema wachezaji wake watacheza kwa tahadhari kesho katika mchezo wao dhidi ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kutokana na historia ya timu hizo zinapokutana.

Kocha wa timu ya Taifa ya Kilimanjaro, Ammy Ninje

Akizungumza na gazeti hili jijini hapa jana, Ninje, alisema kuwa watashuka uwanjani wakijipanga kucheza kwa ushindani kama wanavyojiandaa katika mechi nyingine na wakati wote anawakumbusha nyota wake kuwaheshimu wapinzani.

Ninje alisema jana jioni alitarajia kutumia nafasi nyingine ya "kuwachunguza" Zanzibar Heroes wakati wanavaana na Rwanda (Amavubi) na anaamini atapata mbinu za kuwadhibiti na hatimaye kuondoka na ushindi watakapokutana.

"Hakuna mechi rahisi, najua tunapokutana na Zanzibar huwa kuna ushindani wa kihistoria, tunalijua hilo na tunalifanyia kazi huku tukirekebisha makosa yaliyojitokea katika mechi ya kwanza dhidi ya Libya, kwa kifupi tunakwenda vizuri," alisema Ninje.

Kocha huyo aliongeza kuwa katika mechi ya kesho atamkosa mshambuliaji wake Mbaraka Yusuph ambaye ni majeruhi, lakini hana wasiwasi na safu ya ushambuliaji iliyobakia.

"Mbaraka hatacheza keshokutwa (kesho), tunampumzisha ili apone vizuri, na ana nafasi ya kurejea katika mechi nyingine itakayofuata, watu wote wanajua ushindani dhidi ya Zanzibar, lakini mimi nataka kuwabadilisha na tuanze kupata matokeo mazuri sasa," aliongeza kocha huyo.

Alisema anafurahishwa na juhudi binafsi zinazoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo kuanzia mazoezini na wanapokuwa mchezoni na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yatachangia kuleta mafanikio kwenye timu na katika mchezo wa soka kwa ujumla.

Baada ya kucheza na Zanzibar Heroes kesho, Kilimanjaro Stars ambayo ilianza kwa kutoka suluhu na Libya, itashuka tena uwanjani Jumamosi kucheza na Rwanda na itamaliza mechi zake za hatua ya makundi Jumanne kwa kuvaana na wenyeji Kenya (Harambee Stars).

Mechi ya fainali ya mashindano hayo itafanyika Desemba 17 mwaka huu na kila kundi litatoa timu mbili zitakazosonga mbele kucheza hatua ya nusu fainali.