Ninje: Matokeo  Kili Stars sahihi

05Dec 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Ninje: Matokeo  Kili Stars sahihi

KOCHA wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Ninje, amesema matokeo waliyoyapata kwenye mchezo wao wa kwanza wa michuano ya Cecafa dhidi ya Libya yalikuwa sahihi kutokana na uwezo wa wapinzani wao.

Kocha wa Kilimanjaro Star, Ammy Ninjee

Stars juzi jioni ililazimishana sare na Libya baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo uliochezwa mjini Machakos, Nairobi nchini Kenya.

Ninje aliiambia Nipashe kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu na wenye upinzani, lakini walijitahidi kutengeneza nafasi ila hawakuwa makini kuzitumia.

“Lakini hata Libya walitengeneza nafasi kama sisi, mchezo ulikuwa mgumu na kwa namna ulivyokuwa matokeo haya ni sahihi,” alisema Ninje.

Alisema kuwa upo upungufu aliyouona kwa upande wa timu yake kwenye mchezo na amepanga kutumia siku mbili kuufanyia kazi.

“Ukiangalia kipindi cha kwanza, sehemu ya katikati hatukuwa vizuri, viungo hawakuwa shapu katika kupokea mipira kutoka kwa mabeki na kutawanya kwa washambuliaji, lakini hilo nililiona na nilipofanya mabadiliko timu ilitulia, ni jambo ambalo naenda kulifanyia kazi kwa ajili ya mchezo ujao,” alisema Ninje.

Alisema kuwa ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele ni lazima wapambane kushinda kwenye mchezo wao wa pili.

“Kwa sasa bado tupo kwenye nafasi ya kusonga mbele, kikubwa ni lazima tushinde kwenye mchezo wetu ujao tunajipanga kufanya hivyo,” aliongezea kusema Ninje.

Stars ipo kwenye Kundi A la michuano hiyo pamoja na timu za Kenya, Rwanda na Zanzibar.Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, wenyeji wa michuano hiyo, Kenya walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Rwanda.