Niyonzima: Naiona Simba fainali Caf

21Mar 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Niyonzima: Naiona Simba fainali Caf
  • ***Asema hatimaye sasa ndoto zake zinakwenda kutimia, huku akitoa sababu ya kiwango kurejea...

WAKATI Simba jana usiku ikifahamu mpinzani wake katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kiungo wa kimataifa wa timu hiyo ambaye amerejea katika kiwango chake, Haruna Niyonzima, amesema kikosi chao msimu huu kina uwezo wa kutinga fainali za mashindano hayo yenye utajiri mkubwa kwa ..

ngazi ya klabu barani Afrika.

Akizungumza na gazeti hili jana, Niyonzima alisema timu yao ina kikosi kizuri na tayari wameshafahamu njia za kupata mafanikio kutokana na changamoto walizopitia kwenye hatua ya makundi.

Niyonzima alisema hakuna jambo lisilowekezana katika mchezo wa soka na Simba imefanikiwa kufika hatua hiyo ya robo fainali kutokana na wachezaji kuonyesha bidii na wala hawajabahatisha.

Alisema ndoto zake tangu akiwa mtoto ilikuwa ni kupata nafasi ya kucheza fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na anaamini huenda hilo likatimia msimu huu akiwa na Simba kutokana na kasi na kiu ambayo wachezaji wote wanayo, huku wakiona wana deni mbele ya mashabiki wao.

"Inshaallah, tutacheza fainali kwa sababu tuna kikosi imara na mashabiki wetu hawajawahi kuacha kutushangilia," alisema kiungo huyo wa zamani wa APR ya Rwanda na Yanga ya jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa siri ya kiwango chake kurejea katika ubora wake imetokana na kufanya mazoezi ya nguvu kila siku na hiyo ndiyo imesababisha kuisaidia timu kila anapopata nafasi.

"Sitaki kuona ninawaangusha mashabiki wa Klabu ya Simba, mamilioni ya Watanzania na taifa langu ninalolipenda la Rwanda, kwa sababu hiyo huwa ninaiambia nafsi yangu kuwa nitacheza kwa moyo wangu wote, " aliongeza nyota huyo.

Niyonzima alionyesha kiwango cha juu alipoingia akitokea benchi katika mechi dhidi ya AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na juzi pia wakati Simba wakiikabili Ruvu Shooting katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo walipata ushindi wa mabao 2-0.

Kiungo mwingine wa Simba aliyerejea katika kiwango chake ni Mzambia Clatous Chama ambaye makali yake yalianza kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ugenini kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Lipuli.

Chama ambaye alifunga bao la tatu lililowaondoa Nkana FC katika mechi ya mkondo wa pili ya kuwania kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1, pia alitupia la ushindi walipoichapa AS Vita 2-1, hivyo kuivusha Simba hatua ya robo fainali, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa