NMB yanogesha mashindano ya Gofu Lugalo

09Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
NMB yanogesha mashindano ya Gofu Lugalo

BENKI ya NMB imetoa Sh. milioni 60, kwa ajili ya kudhamini mashindano maalumu ya Mchezo wa Gofu ya Mkuu wa Majeshi 'NMB CDF Trophy 2021', yanayotarajiwa kuanza Septemba 17  hadi 19, mwaka huu kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu vya Lugalo jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Maalum Benki ya NMB, Getrude Mallya akimakabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh.milioni 25.5 Mwenyekiti wa Klabu ya Golf ya Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Michael Luwongo ikiwa ni udhamini wa Mashindano ya Mchezo wa Golf ya Mkuu wa Majeshi 'NMB CDF Trophy 2021'. Kulia ni Meneja wa Club ya Golf ya Lugalo, Luteni Kanali, Frank Kaluwa na Meneja Mwandamizi Wateja Maalum wa NMB, Emmanuel Mahodanga wakishuhudia. Benki ya NMB imetoa takribani milioni 60 kwa ajili ya udhamini wa mashindano hayo kiujumla kwa mwaka huu.

Mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka, lengo kuu ni kuuinua mchezo huo pamoja na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi, ili kuja kuwa tegemeo kwa taifa kwa siku zijazo.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi hundi ya udhamini huo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Maalumu wa NMB, Getrude Mallya,  alisema wanajisikia furaha kuwa sehemu ya kufanikisha kufanyika kwa mashindano hayo, ambayo anaamini mwaka huu yatafana kutokana na zawadi nono, ambazo zimeandaliwa kwa washindi.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Maalum Benki ya NMB, Getrude Mallya (katikati) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kwenye hafla ya kupokea mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 25.5 kwa ajili ya udhamini wa Mashindano ya Mchezo wa Golf ya Mkuu wa Majeshi 'NMB CDF Trophy 2021'. Kulia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Golf ya Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo pamoja na Meneja Mwandamizi Wateja Maalum wa NMB, Emmanuel Mahodanga (kulia) wakishuhudia.

Mallya alisema kiasi hicho cha fedha kimetumika katika kununua vifaa mbalimbali vitakavyotumiwa na washiriki wa shindano hilo ikiwamo fulana, kofia, bendera na zawadi za washindi, ambazo zitatolewa siku ya mwisho.

“Sisi kama NMB tunajisikia furaha kuona shindano la mwaka huu linakwenda kufanyika kwa ubora na mafanikio ya juu kabisa na hii inathibitisha kwamba sisi ndio Benki, ambayo inaijali jamii kwa ukaribu kutokana na kudhamini masuala mbalimbali ikiwamo ya kimichezo,” alisema Mallya.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Michael Luwango, alisema zaidi ya wachezaji 170, wanatarajia kushiriki mashindano ya mwaka huu ikiwamo vijana wadogo wa shule (Junior), ambao wao ndio watakaofungua mashindano hayo siku ya kwanza Septemba 17, mwaka huu.

“Siku ya ufunguzi itakuwa kwa vijana wadogo Junior) unajua wameanza mitihani sasa wakitoka huko vichwa vimechemka, wanaweza kuyatumia mashindano haya kujipooza na siku itakayofuata, ambayo ni Septemba 18 na 19 ndio itakuwa zamu ya wakubwa na wale wachezaji wakimataifa endapo watajisikia ilimradi kufuata taratibu zinazotakiwa ikiwamo kulipa ada,” alisema Luwango huku akieleza mkapa sasa waliomba na kuthibitisha kushiriki wamefikia 100 kutoka klabu 10 tofauti nchini.

Naye Katibu wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Boniface Nyiti, alisema shindano hilo la Mkuu wa Majeshi lipo kwenye Kalenda ya TGU na limekuwa na mchango mkubwa kwa taifa kutokana na kutoa wacheaji wengi, ambao wanajenga timu ya taifa.