NMB yaipiga tafu Balaza la Wawakilishi

11Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
NMB yaipiga tafu Balaza la Wawakilishi

TIMU ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepokea jezi za mpira wa miguu pamoja na mpira wa kikapu kutoka kwa Benk ya NMB tawi la Zanzibar ili kuisaidia timu hiyo.

Spika wa Baraza la wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid (kulia), akipokea moja ya vifaa vya michezo kutoka kwa Mwakilishi wa NMB, Mkaguzi Mkuu wa ndani wa benki hiyo, Juma Kimori. PICHA: MARTIN KABEMBA

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Jezi hizo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zuberi Ali Maulid aliiomba benki hiyo kuendelea kuisaidia Serikali hususani katika suala zima la kukuza michezo hapa visiwani.

Alisema Zanzibar kuna vipaji mbalimbali vya michezo hivyo vinahitaji kuendelezwa ikiwemo kusaidiwa vifaa pamoja na kupata misaada mbalimbali ya kukuza vipaji hivyo.

“Zanzibar kuna vipaji hususani vya mpira wa miguu, lakini  muda mwingine wanakumbwa na Changamoto za vifaa vya kimichezo hivyo  NMB wanaweza kuwasaidia kwa kuangalia changamoto zao kama mipira na vifaa vingine vya michezo” . Alisema

Aidha alisema Baraza la Wawakilisha litaendelea kuthamini juhudi zinazofanywa na Benk ya NMB katika kusaidia mambo mbalimbali ya maendeleo ya Zanzibar iwe sekta ya michezo na hata sekta nyingine ambazo zimesaidia.

Hata hivyo, ameitaka benki hiyo kufunga mashine ya kutolea Pesa (ATM) katika  eneo la Baraza hilo ili kuwarahisishia huduma wawakilishi wanaotumia benki hiyo pamoja na wananchi wanaokaa maeneo jirani na baraza hilo.

Kwa upande wake, Meneja mwandamizi Idara ya Huduma na Mahusiano ya Serikali wa benki hiyo kutoka Makao Makuu ya benki hiyo, Adelard Mang’ombo alisema Benki hiyo inautaratibu wa kurudisha fadhila kwa wateja wao ikiwemo kutoa misaada kwa jamii inayowazunguka hivyo wameona ipo haja ya kushiriki katika michezo katika kipindi hiki ,

Alisema kuwa Benk ya NMB itaendelea kuisaidia Serikali katika suala la kukuza michezo katika jamii kwani ushiriki wa michezo ni moja ya mambo ambayo yanasaidia kukuza Afya na hata kujiepusha na maradhi ambayo yanasababishwa na kutoshiriki mazoezi.

Aidha, Meneja wa Biashara za Serikali kutoka benki hiyo, Abdallah Duchi, alisema Benki hiyo itaendelea kuwekeza Zanzibar pamoja na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika nyanja ya ukusanyaji wa mapato na hata kwa kuzisaidia timu za Zanzibar katika suala la michezo kupitia wizara husika.