NMB yamwaga mil.25 michuano ya Golf- Lugalo

23Sep 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
NMB yamwaga mil.25 michuano ya Golf- Lugalo

Benki ya NMB imetoa udhamini wa Shilingi milioni 25 kwaajili ya Mashindano ya Gofu ya Mkuu wa Majeshi Tanzania (NMB CDF Trophy 2022), kama muendelezo wa sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Septemba 1.

Kutokana na sababu mbalimbali mashindano hayo kwa mwaka huu yamesogezwa hadi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza wakati akipokea mfano wa hundi iliyotolewa na benki hiyo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo, aliishukuru NMB kwa kuwa mdhamini wa muda mrefu na kufanyia maboresho zaidi kwa mwaka huu huku akiweka wazi kuwa timu mbalimbali zimethibitisha kushiriki michuano hiyo, ambayo itahusisha watoto (junior), madaraja (division) ya A, B, na C, pamoja na wanawake na 'Seniors'.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Wateja Maluum wa Benki ya NMB, Getrude Mallya, alisema benki hiyo imedhamini mashindano hayo kwa Sh. milioni 25 huku akiwaalika viongozi wa klabu ya Gofu Lugalo kushiriki mbio za NMB Marathon 2022  ‘Mwendo wa Upendo’ zitakazofanyika Oktoba 1 mwaka huu katika Viwanja vya Leaders Club kwa lengo la kukusanya Sh. mil. 600 za kusaidia matibabu ya kina mama wenye matatizo ya fistula nchini.

Mashindano ya Gofu yatafanyika Oktoba 1 hadi 2 mwaka huu kwenye Viwanja vya Gofu Lugalo, jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa