NMB yatoa Mfungaji Bora BBL 2018/19

21Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
NMB yatoa Mfungaji Bora BBL 2018/19

NYOTA wa kikapu wa kikosi cha Benki ya NMB, Kaikai Leka, ameibuka Mfungaji Bora (Best Scorer) wa Ligi ya Kikapu kwa Taasisi za Fedha (Bankers Basketball League - BBL 2018/19), baada ya kufunga pointi 160 katika mechi za michuano hiyo iliyofikia tamati jana, jijini Dar es Salaam.

Katika fainali ya kukata na shoka iliyopigwa kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam jana, Benki ya DTB iliibuka mshindi baada ya kuifunga NMB kwa pointi 90-73, huku Leka akifunga zaidi ya nusu ya pointi zao, hivyo kutangazwa Mfungaji Bora akifuatiwa na Acram Majid wa DTB, aliyefunga pointi 129.

Leka alizawadiwa Tuzo ya Mfungaji Bora, kama ilivyokuwa kwa Mchezaji Bora (MVP) Leonard Benedict wa DTB, Beki Bora Frank Mwemezi wa DTB na kinara wa kufunga pointi tatu kwa mtupo mmoja (Leading Three Pointer), Acram Majid aliyefanya hivyo mara 13 katika michuano yote.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi na kufunga mashindano, Mratibu wa BBL 2018/19, Gozbert Boniface, alizipongeza timu sita zilizoshiriki michuano hiyo kwa upande wa mpira wa kikapu na kuzitaka kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao, utakaoanza baadaye mwaka huu.

“Tunaipongeza DTB kwa kutwaa taji, lakini pia kwa NMB kwa kutwaa medali za fedha za ushindi wa pili na pia kwa kutoa Mfungaji Bora wa michuano hii, iliyoshirikisha benki sita za NMB, DTB, Azania, CRDB, TADB na NBC,” alisema Boniface wakati akitoa neno la shukrani.

Kwa upende wake, mgeni rasmi wa fainali hiyo, Juma Kimori, ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa NMB, aliwapongeza waratibu kwa wazo zuri la kuanzisha michuano hiyo, iliyoimarisha uhusiano baina ya taasisi za kifedha nchini, huku akiwapongeza mabingwa na washindi wa pili.

Habari Kubwa