Nnauye atia neno Yanga, Azam FC

22Mar 2016
Nipashe
Nnauye atia neno Yanga, Azam FC

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo Nape Nnauye amezitaka Yanga na Azam FC kukaza buti kutokana na kufikia hatua ngumu kwenye michuano ya Afrika.

Nape Nnauye.

Baada ya timu hizo kusonga mbele, Yanga itacheza dhidi ya Al Ahly ya Misri, wakati Azam watapepetana na Esperance ya Tunisia.

Yanga ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 dhidi ya APR ya Rwanda, wakati Azam wakiifunisha virago Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa mabao 7-3.

Akizungumza baada ya mechi ya Azam Nnauye, alisema timu za Uarabuni zimekuwa na kawaida ya kuzisumbua timu za Tanzania, hivyo wawakilishi hao ni lazima kuanza kujiandaa mapema.

"Yanga na Azam wote wanajua ugumu wa timu hiyo na katika maandalizi watakayofanya wazingatie kwa kina uwezo wa timu hizo," alisema Nnauye.

Aliwataka wachezaji na viongozi wa timu hizo kutobweteka na ushindi waliopata kwenye mechi za awali, badala yake ushindi huo uwe chachu ya kufanya vizuri kwenye mechi zijazo.

Alisema kutokana na hilo, timu hizo zinapaswa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani ili iwe rahisi kupita katika mechi ya marudiano ambayo itakuwa ugenini.

"Nawaombeni mjiandae vizuri, hatua mliyofikia kwa sasa ni ngumu bila maandalia ya kutosha hamtaweza kusonga mbele," alisema waziri huyo wenye dhamana ya kusimamia michezo.

Habari Kubwa