Nsajigwa: Hakuna mechi rahisi VPL

27Feb 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nsajigwa: Hakuna mechi rahisi VPL

HUKU timu yake ikiwa imekata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA, Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, amesema kuwa hakuna mechi rahisi katika mashindano hayo au Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inaelekea ukingoni.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa.

Nsajigwa aliliambia gazeti hili jana kuwa kila mechi kwao ni sawa na fainali na wanawapongeza wachezaji wao kwa kucheza kwa bidii ili kusaka matokeo mazuri ambayo yamewafanya wasonge mbele katika michuano hiyo ambayo bingwa mtetezi Simba alishaondolewa.

Beki na nahodha huyo wa zamani wa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa alisema kuwa kadri mashindano ya Kombe la FA yanavyosonga mbele na Ligi Kuu, ndiyo ushindani huongezeka na amewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuendelea kushirikiana na viongozi ili watimize malengo ya kutetea ubingwa wanaoushikilia.

"Napenda kuwapongeza wachezaji wetu kwa juhudi walizozionyesha kwa sababu mechi ilikuwa ngumu, Majimaji walikuwa nyumbani kwao na wametupa ushindani mkubwa, lakini nashukuru vijana walipambana wakapata mabao ambayo yametusaidia tunasonga mbele katika mashindano haya," alisema Nsajigwa.

Naye Kocha Msaidizi wa Majimaji, Peter Mhina, alisema kuwa makosa waliyofanya wachezaji wake ndiyo yaliwapa faida Yanga ya kupata mabao hayo lakini waliwazidi kiwango.

"Makosa na uzembe wa wachezaji wangu ndio umeisaidia Yanga, tumetoka katika mashindano ya FA lakini bado tutapambana kuhakikisha hatushuki daraja kwenye Ligi Kuu," alisema kocha huyo.

Yanga ilirejea jijini Dar es Salaam jana tayari kuanza maandalizi ya safari ya kueleka Mtwara kuifuata Ndanda FC kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika kesho kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona ulioko mkoani humo.

Mabingwa hao watetezi wenye pointi 37 wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakati wenyeji wao wako katika nafasi ya 13 wakiwa na pointi 18 huku Kagera Sugar, Majimaji na Njombe Mji kila moja ikiwa na pointi 15 zikiburuza mkia.

 

Habari Kubwa