Ntibazonkiza awatoa Yanga wasiwasi J'mosi

03May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ntibazonkiza awatoa Yanga wasiwasi J'mosi

KUELEKEA mechi ya watani wa jadi dhidi ya Simba, mshambuliaji tegemeo wa Yanga, Said Ntibazonkiza, amewatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo baada ya kueleza kwamba anaamini watapata matokeo.

Katika michezo miwili iliyopita wakati wakipokea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Azam FC kwenye Ligi Kuu na kisha kwenda kupata ushindi kama huo dhidi ya Tanzania Prisons hatua ya 16-bora ya Kombe la FA, Ntibazonkiza amekuwa chaguo la kwanza chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ambaye ameiongoza timu hiyo kwenye mechi hizo.

Kiungo huyo mshambuliaji raia wa Burundi amekuwa na uwezo mkubwa wa kucheza na mpira na kupiga mipira ya adhabu akisaidiaina na Carlos Carlinhos.

"Sifuatilii mechi za wapinzani wangu hao, mimi sijui ila kikubwa tunachoangalia ni mechi zetu na kuona tunapata matokeo, hakuna jambo lingine.

"Kuhusu kucheza sina wasiwasi pale ambapo ninapata nafasi hivyo ni suala la kusubiri na kuona itakuaje," alisema.

Kama Ntibazonkiza atacheza itakuwa mechi yake ya kwanza dhidi ya watani hao wa jadi, Simba kuichezea Yanga.

Simba yenye alama 61 na mechi mbili mkononi, ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiizidi Yanga kwa pointi tatu.

Habari Kubwa