Ntibazonkiza: Yanga itang'ara

08Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ntibazonkiza: Yanga itang'ara
  • ***Yajipanga kurejea na kasi pamoja na nguvu mpya ili kumaliza...

WAKATI kikosi cha Yanga kikitarajia kurejea uwanjani keshokutwa kuendelea na mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa timu hiyo, Saido Ntibazonkiza amesema mashabiki wasiwe na hofu kwa sababu nia na nafasi ya kutwaa ubingwa wanao.

Yanga inatarajia kushuka dimbani keshokutwa kuwakabili KMC FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ntibazonkiza alisema hakuna timu wanayoihofia katika ligi hiyo inayokaribia ukingoni na kila siku kikosi chao kinajiimarisha ili kusaka pointi tatu kwenye kila mechi watakayocheza.

Ntibazonkiza alisema mashabiki na wanachama wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi kwa sababu wachezaji wote wamejipanga kupambana katika kila mechi ili kujiimarisha kwenye uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 18 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Nyota huyo alisema anaendelea vizuri na mazoezi na amepewa programu maalum kabla ya baadaye kuungana na wachezaji wenzake katika mazoezi ya pamoja.

"Ninaamini nitakuwa na kipindi kingine kizuri, kwa sasa niko fiti, ninamshukuru Mungu, mengine yataonekana kwa vitendo uwanjani, kikubwa ni kuwa na afya njema," alisema kiungo huyo ambaye awali kabla ya ligi haijasimama alikosekana ndani ya kikosi cha Yanga kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na kuuguza maumivu ya nyonga.

Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi, aliliambia gazeti hili anaamini kikosi chake kitaendelea kupata matokeo chanya katika mechi zake tano zinazofuata ambazo zitachezwa hapa jijini.

Mwambusi alisema Yanga imekuwa na rekodi nzuri kwenye uwanja huo na mapumziko yaliyomalizika waliyatumia kurekebisha upungufu mbalimbali na sasa watarejea na nguvu mpya.

"Timu inaendelea vizuri na maandalizi kuelekea mchezo wa ligi dhidi ya KMC, tunajua mechi haitakuwa rahisi, tunakutana na moja ya timu zinazotoa ushindani na zenye rekodi nzuri pia, wachezaji wote wako vizuri na wanaendelea kujiimarisha, Saido ameshaanza mazoezi lakini alikuwa katika programu maalum," alisema Mwambusi.

Aliongeza kikosi cha Yanga kimeendelea kuimarika na kiu ya mafanikio ambayo kila mchezaji anayo, inasaidia kuongeza ubora wa timu.

"Kila mmoja anataka kuonyesha wamedhamiria kusaka ubingwa, ushindani unaonekana mazoezi ni dalili nyingine nzuri za kuelekea kwenye mafanikio, utulivu na umakini ukiwepo, hakika tutafikia kile tunachokihitaji," Mwambusi alisema.

Baada ya mechi hiyo ya keshokutwa, Yanga itaendelea kubakia jijini kucheza dhidi ya Biashara United ifikapo Aprili 17, mwaka huu na siku tatu baadaye itawaalika Gwambina FC wakati Aprili 23, mwaka huu wataivaa Azam FC huku mchezo wake wa nne mfululizo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Habari Kubwa