Nyoni aikosa Guinea sasa arejeshwa Dar

26Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Nyoni aikosa Guinea sasa arejeshwa Dar

WAKATI Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kesho ikishuka katika Uwanja wa Reunification/Douala nchini Cameroon kuvaana na Guinea kwenye mechi yake ya mwisho ya Kundi D ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), itaendelea kumkosa beki wake mkongwe, Erasto Nyoni, imeelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Cliford Ndimbo, kutoka Cameroon jana, ilieleza kuwa jopo la madaktari limemruhusu Nyoni kurejea nyumbani kuendelea na matibabu zaidi.

"Mchezaji Erasto Nyoni, amepewa ruhusa ya kuondoka kwenye Kambi ya Taifa Stars, amerudi nyumbani kuendelea na matibabu baada ya kushauriwa na jopo la madaktari wa timu," ilieleza taarifa hiyo.

Katika mechi hiyo itakayopigwa majira ya saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, Stars inahitaji ushindi ili kutinga hatua ya robo fainali huku Guinea yenyewe sare yoyote ikiivusha hatua hiyo kutokana na kuongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne sawa na Zambia ambayo nayo itashuka dimbani muda huo dhidi ya waburuza mkia wa kundi lao, Namibia.

Zambia inazidiwa na Guinea kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa tu, huku Taifa Stars yenyewe ikiwa na pointi tatu baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa mabao 2-0 dhidi ya Wazambia hao na kisha kuwachapa Namibia bao 1-0.

Habari Kubwa