Nyoni atwaa tuzo ya mchezaji bora Simba

03Nov 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Nyoni atwaa tuzo ya mchezaji bora Simba

BEKI wa pembeni wa klabu ya Simba ambaye pia anamudu kucheza namba nyingi uwanjani, Erasto Nyoni, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Oktoba wa klabu hiyo.

Erasto Nyoni.

Nyoni, ameshinda tuzo hiyo baada ya kufanya vizuri ndani ya kikosi cha Simba katika mwezi Oktoba akiisaidia timu yake kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu.

Pamoja na ukongwe wake kwenye ligi, Nyoni amekuwa akifanya kazi nzuri na hata kuwashinda baadhi ya wachezaji vijana ndani ya kikosi hicho.

Taarifa ya klabu ya Simba imeeleza kuwa Nyoni amekuwa na mchango mkubwa ndani ya timu hiyo na pamoja na umri wake amekuwa sehemu ya mhimili wa timu hiyo.

Kwa tuzo hiyo, Nyoni atapatiwa kiasi cha Shilingi 500,000 pamoja na kuingia kwenye kundi la wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa klabu hiyo.

Nyoni alijiunga na Simba mwezi Julai mwaka huu akitokea kwenye kikosi cha Azam FC ambapo alidumu na timu hiyo kwa zaidi ya miaka sita.

Nyoni alijiunga na Azam mwaka 2010 akitokea kwenye klabu ya Vital'O ya Burundi aliyojiunga nayo akitokea AFC ya Arusha.