Nyoni: Ushindi Yanga ulijulikana

01May 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nyoni: Ushindi Yanga ulijulikana

SHUJAA wa Simba dhidi ya Yanga, Erasto Nyoni, ameweka wazi kuwa alifahamu timu yake itaibuka na ushindi katika mchezo wa juzi dhidi ya watani wao hao.

Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 huku Nyoni akifunga bao hilo pekee lililoipa Simba pointi zote tatu muhimu.Akizungumza na Nipashe jana, Nyoni, alisema amekuwa na furaha baada ya kufunga bao hilo na kusema tangu awali walikuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

"Nilifahamu mapema tutashinda mchezo ule, lakini sikufikiria kama nitafunga, tulipanga kupambana kuhakikisha tunashinda, ushindi huu ni wa Wanasimba wote," alisema Nyoni aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Azam FC.

"Mchezo na Yanga umepita, sasa tunajipanga kwa mchezo ujao, tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi kwenye michezo yote iliyobaki," aliongeza kusema Nyoni.

Bao alilolifunga Nyoni juzi linakuwa la tatu msimu huu kuifungia Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, ambayo pia inaidhamini Yanga.

Kwa ushindi wa juzi, Simba sasa itatakiwa kushinda michezo miwili tu kuweza kutawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.

Endapo Simba itashinda mechi hizo mbili, itafanikiwa kutwaa ubingwa bila kupoteza na kabla ligi haijamalizika kama ilivyofanya Barcelona ya Hispania juzi. 

Habari Kubwa