Nyota Yanga walia ratiba ya ligi

12May 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Nyota Yanga walia ratiba ya ligi

BAADA ya kushuhudia wakiutema rasmi ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara juzi kwa kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tanzania Prisons, baadhi ya wachezaji wa Yanga wamesema ratiba ngumu ya ligi hiyo ndio chanzo cha kufanya vibaya.

beki wa pembeni wa Yanga, Juma Abdul.

Yanga juzi ikiwa ugenini ilikubali kipigo hicho kutoka kwa Tanzania Prisons na kuiacha Simba ikitangaza ubingwa kabla ya kucheza mchezo wake wa leo dhidi ya Singida United.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, beki wa pembeni wa Yanga, Juma Abdul, alisema kuwa ratiba iliwabana zaidi na kuepelekea wachezaji wengi kuwa na uchovu.

Alisema hawakuwa na muda wa kupumzika pindi wanapotoka kwenye michezo yao ya kimataifa.

"Hata mchezo wa leo (juzi) tumecheza tukiwa na uchovu kwa sababu tulipotoka Algeria tuliunganisha kuja Mbeya, ratiba imechangia sisi kufanya vibaya kwenye michezo yetu ," alisema.

Kauli hiyo pia iliungwa mkono na mshambuliaji wa timu hiyo, Emmanuel Martin, ambaye alisema uchovu umewapa nafasi Tanzania Prisons kuibuka na ushindi.

Matokeo hayo ya juzi yameifanya Yanga kusalia kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 48, pointi moja pungufu ya Azam FCwanaoshika nafasi ya pili huku mabingwa wapya, Simba wakiwa na pointi 65.