Penalti iliyokoswa na Gabriel Martinelli ilipelekea washikabunduki hao kutolewa katika mechi ya mkondo wa pili ya hatua ya 16 bora kwenye Uwanja wa Emirates, baada ya kutoka ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza.
Matokeo hayo yanamaanisha Arsenal sasa wameshindwa kushinda mechi yoyote kati ya tano za mwisho za mtoano wakiwa nyumbani kwenye Ligi ya Europa tangu walipoifunga Valencia Mei, mwaka 2019.
Macho yote sasa yatakuwa katika kampeni ya Ligi Kuu England, ambapo Arsenal wanaogoza kwa pointi tano dhidi ya Manchester City zikiwa zimesalia mechi 11 kuchezwa, na Odegaard anataka timu yake kujibu mapigo dhidi ya Crystal Palace hapo kesho.
"Nadhani tulifanya vya kutosha katika baadhi ya vipindi vya mchezo lakini mechi nyingi hatukuwa katika kiwango ambacho tunapaswa kuwa," alisema akiiambia BT Sport.
"Sehemu ya mchezo tulifanya vizuri, katika mchezo mzima, hatukucheza soka letu bora zaidi. Ulikuwa mchezo mgumu mwishoni.
"Ni timu nzuri, tulijua hilo, tulijua sifa zao, na tulijiandaa, lakini nadhani ilikuwa zaidi juu yetu leo (juzi).
"Hatukucheza jinsi tunavyofanya kawaida, na labda hatukuweka nguvu kama kawaida. Hiyo inakatisha tamaa lakini sasa tunapaswa kuangalia mbele na kuwa tayari kwa Jumapili.
“Lazima tukumbuke umekuwa msimu mzuri sana, tumefanya mambo ya ajabu mwaka huu, bila shaka ni pigo kubwa kutoka kwenye mashindano haya, lilikuwa ni lengo kubwa kwetu, lakini tunatakiwa kutazama mbele.
“Lazima tuangalie Jumapili, turudi kwa nguvu zaidi na kuhakikisha tunamaliza vizuri kwenye ligi, hilo ndilo jambo pekee tunaloweza kufanya kwa sasa.”